OIC yaitaka Israel ikabidhi maeneo yote iliyoghusubu ikiwemo Golan
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imeutaka utawala wa Kizayuni wa Israel ukabidhi maeneo yote ulioyaghusubu ikiwemo Miinuko ya Golan ya Syria.
OIC imeyasema hayo katika barua yake kwa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, utawala huo ghasibu unapaswa kuondoka mara moja katika ardhi zote ulizozipora.
Katika barua hiyo kwa Michelle Bachelet, mshirikishi wa ngazi za juu wa OIC, Taher Hussein Andaraabi ameeleza juu ya wasiwasi mkubwa ilionayo taasisi hiyo, kwa hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuitambua Miinuko ya Golan ya Syria kuwa milki ya utawala haramu wa Israel.
Barua hiyo ya OIC imerejelea azimio nambari 40/21 la Ofisi ya Haki za Binadamu ya UN, pamoja na maazimio nambari 242, 338, na 497 ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambayo kwa pamoja yanasisitiza kuwa, Miinuko ya Golan ni mali halali ya Syria.
Utawala wa Kizayuni wa Israel uliivamia na kuiteka Milima ya Golan ya Syria mwaka 1967. Eneo hilo lina ukubwa wa takriban kilomitamraba 200.
Hivi karibuni Rais Donald Trump wa Marekani alitekeleza vitisho vyake, kwa kusaini eti azimio la kuitambua miinuko ya Golan ya Syria kuwa mali ya utawala wa Kizayuni wa Israel, hatua ambayo imeendelea kukosolewa na kulaaniwa katika kila kona ya dunia hususan katika Ulimwengu wa Kiislamu.