Syria: Magenge ya kigaidi yameharibu maelfu ya maeneo ya kihistoria
Idara ya Majumba ya Makumbusho na Athari za Kihistoria ya Syria imetangaza kwamba, kwa akali maeneo elfu 10 ya kihistoria ya nchi hiyo yako katika hatari ya kutokomezwa na kuporwa.
Mahmoud Hamud, Mkuu wa Idara ya Majumba ya Makumbusho na Athari za Kihistoria nchini Syria amesema hayo leo na kubainisha kwamba uchimbaji mashimo ulio kinyume cha sheria, umetokomeza athari nyingi za kiutamadunia za nchi hiyo ya Kiarabu. Ameongeza kwamba kwa akali athari milioni moja za kihistoria zimetorosha nje ya Syria kupitia mipaka hususan mipaka ya pamoja ya Uturuki, Jordan na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Mzozo wa Syria uliibuka mwaka 2011 baada ya makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Saudi Arabia, Marekani na washirika wao kuivamia nchi hiyo ya Kiarabu kwa lengo la kuleta mabadiliko katika eneo la Asia Magharibi kwa maslahi ya utawala khabithi wa Kizayuni.
Hata hivyo jeshi la Syria kwa kusaidiwa na washauri wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa uungaji mkono wa Russia, lilifanikiwa kulishinda kundi la kigaidi la Daesh (ISIS). Mbali na hayo jeshi la Syria linaendelea na juhudi za kuyasambaratisha mabaki ya kundi hilo.