Syria yaushtaki utawala wa Kizayuni wa Israel Umoja wa Mataifa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i54499-syria_yaushtaki_utawala_wa_kizayuni_wa_israel_umoja_wa_mataifa
Syria imemwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa Baraza la Usalama la Umoja huo ikilaani mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya nchi hiyo na kusema uchokozi huo ni sehemu ya njama za Tel Aviv za kutaka kurefusha mgogoro nchini Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 02, 2019 03:14 UTC
  • Syria yaushtaki utawala wa Kizayuni wa Israel Umoja wa Mataifa

Syria imemwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa Baraza la Usalama la Umoja huo ikilaani mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya nchi hiyo na kusema uchokozi huo ni sehemu ya njama za Tel Aviv za kutaka kurefusha mgogoro nchini Syria.

Alfajiri ya Jumatatu ya jana utawala wa Kizayuni wa Israel uliyashambulia kwa maroketi baadhi ya maeneo ya mji mkuu wa Syri,a Damascus na mji wa Homs huko katikati mwa Syria na kuua raia wanne akiwemo mtoto mmoja mchanga.

Katika barua hizo mbili Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litekeleze majukumu yake na kuchukua hatua za kuwazuia Wazayuni kukariri ukiukaji wa sheria za kimataifa na hati ya Umoja wa Mataifa.

Syria imesema mashambulizi hayo yamefanyika kwa shabaha ya kuyasaidia makundi ya kigaidi, kuzuia harakati za jeshi la Syria na waitifaki wake za kuyaangamiza makundi ya Daesh na Jabhatu Nusra na makundi mengine ya kigaidi.

Barua hizo zimesisitiza kuwa uchokozi wa sasa wa Israel haukuweza kuwatia woga watu wa Syria, na kinyume chake, umezidisha azma yao ya kuushinda ugaidi na kukomboa eneo la Golan linalokaliwa kwa mabavu na Israel.

Wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh

Syria imesisitiza kuwa uhasama huo wa Israel unatokana na misaada na uungaji mkono wa Washington na baadhi ya wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Vilevile imelitaka Baraza la Usalama liichukuli hatua Israel kutokana na ugaidi na jinai zote unazofanya dhidi ya mataifa ya Syria na Palestina.