Bin Salman: Vita na Iran vitapelekea uchumi wa dunia uangamie
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i56345-bin_salman_vita_na_iran_vitapelekea_uchumi_wa_dunia_uangamie
Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia Arabia Mohammad bin Salman (MbS) ameonya kuwa, vita na Iran vitapelekea kuangamia kikamilifu uchumi wa dunia. Aidha ametoa wito wa kutatuliwa 'kwa amani' mgogoro na Iran katika kauli ambayo inatafautiana na matamshi yake ya huko nyuma ya kivita na majigambo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 30, 2019 23:18 UTC
  • Bin Salman: Vita na Iran vitapelekea uchumi wa dunia uangamie

Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia Arabia Mohammad bin Salman (MbS) ameonya kuwa, vita na Iran vitapelekea kuangamia kikamilifu uchumi wa dunia. Aidha ametoa wito wa kutatuliwa 'kwa amani' mgogoro na Iran katika kauli ambayo inatafautiana na matamshi yake ya huko nyuma ya kivita na majigambo.

Akizungumza katika mahojiano na televisheni ya CBS ya Marekani, bin Salman ameashiria mgogoro uliopo baina ya nchi yake na Iran na kusema 'suluhisho la kisiasa na la amani ni bora kuliko suluhiso la kijeshi'.

Mrithi wa Ufalme wa Saudia amesema asilimia 30 ya nishati ya dunia inatoka eneo la Ghuba ya Uajemi huku asilimia 20 ya njia za kibiashara duniani zikiwa katika eneo hilo na asilimia 4 ya pato ghafi la dunia (GDP) aidha liko katika eneo hilo. Ameongeza kuwa, kwa kuzingatia nukta hizo, iwapo vita vitaibuka basi dunia itatumbukia katika matatizo makubwa sana.

Bin Salman amesema kuendelea mgogoro katika eneo kunaweza kupelekea bei ya mafuta ya petroli kupanda kwa kiasi ambacho hakijawahi kushuhudiwa.

Wakati huo huo Waziri Msaidizi wa Mambo ya Nje katika Umoja wa Falme za Kiarabu Anwar Gargash naye pia ameonekana kutupilia mbali mitazamo hasimu dhidi ya Iran katika makala aliyoandika katika gazeti la Financial Times Jumapili. Gargash ambaye nchi yake ni muitifaki wa karibu wa Saudia ametoa wito wa kufanyika mazungumzo na Iran ili kupunguza hali ya taharuki. Kauli za Bin Salman na ya Gargash ni kinyume kabisa na matamshi yao ya kichochezo ya huko nyuma dhidi ya Iran.