Guterres asisitiza udharura wa kutumwa misaada ya kibinadamu Syria
-
António Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kutumwa misaada zaidi ya kibinadamu nchini Syria kupitia mipaka ya nchi kavu.
Ripoti iliyotolewa na António Guterres katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imesema kuwa, hakuna chagua bora zaidi kwa ajili ya kupeleka misaada ya kibinadamu nchini Syria kama mipaka ya nchi kavu.
Hii ni katika hali ambayo wanachama wa Baraza la Usalama wanashauriana kuhusu uwezekano wa kurefusha muda wa operesheni ya misaada ya kibinadamu nchini Syria kupitia mipaka ya nchi kavu. Muda wa operesheni hiyo utamalizika mwanzoni mwa mwaka ujao.
Vivuko vinne vya nchi kavu vinatumika kwa sasa kwa ajili ya kutuma misaada ya kibinadamu nchini Syria. Viwili kati ya vivuko hivyo viko katika mpaka wa Syria na Uturuki, kimoja katika mpaka wa nchi hiyo na Jordan na kingine katika mpaka wa Syria na Iraq.
Syria ilitumbukia katika mgogoro mkubwa mwaka 2011 baada ya makundi ya kigaidi yaliyokuwa yakiungwa mkono na kufadhiliwa na Marekani, Saudi Arabia, Israel na waitifaki wao kuvamia sehemu kubwa ya ardhi ya nchi hiyo. Miongoni mwa malengo ya uvamizi huo ni kuindoa madarakani serikali halali ya Syria na kubadilisha mlingano wa nguvu kwa maslahi ya utawala haramu wa Israel.