Mamluki 60 wa Saudia waangamizwa katika shambulizi la Ansarullah Yemen
Makumi ya mamluki wa Saudi Arabia wameuawa katika operesheni iliyofanywa na jeshi la Yemen kwa kushirikiana na harakati ya Ansarullah huko kaskazini mwa Yemen.
Televisheni ya taifa ya Saudia jioni ya jana ilikiri kuwa mamluki zaidi ya 60 waliokuwa wakipigana kwa niaba ya Riyadh wameuawa katika shambulizi la kombora la Ansarullah lililolenga kambi ya kijeshi ya muungano huo vamizi unaoongozwa na Saudia katika mkoa wa Ma’rib wa kaskazini mwa nchi.
Duru za hospitali zimearifu kuwa, wanajeshi 45 wa muungano huo vamizi ni miongoni mwa waliouawa katika shambulio hilo la jana ya Ansarullah, ambayo inatajwa kuwa kubwa zaidi katika wiki za hivi karibuni.
Mapema jana Jumamosi pia, mamluki wengine 12 wa muungano huo wa kijeshi wa Saudia na Imarati huko nchini Yemen waliangamizwa katika operesheni ya wanamapambano wa Ansarullah, katika mkoa wa Hajjah, kaskazini magharibi mwa nchi hiyo maskini ya Kiarabu.
Saudi Arabia na washiriki wake katika vita vya Yemen tokea Machi mwaka 2015 wamekuwa wakishambulia shule, mahospitali, na miundombinu ya nchi hiyo na ripoti za mashirika ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa zimethibitisa kuwa maelfu ya watu wakiwemo wanawake na watoto wameuawa katika mashambulizi hayo ya kinyama.