Katibu Mkuu wa UN atahadharisha kuhusu kushadidi mapigano kaskazini mwa Syria
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuhusu kuongezeka mapigano na mivutano ya kijeshi katika maeneo ya kaskazini magharibi mwa Syria.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric amesema kuwa Katibu Mkuu wa umoja huo Antonio Geterres ameeleza wasiwasi wake kuhusiana na ongezeko la machafuko na mivutano ya kijeshi katika maeneo ya kaskazini magharibi mwa Syria na ametoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano katika maeneo hayo.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Umoja wa Mataifa imesema: Guterres ameyataja mashambulizi yanayofanywa dhidi ya raia na miundombinu nchini Syria kuwa ni jambo lisilokubalika.
Rupoti zinasema kuwa, magaidi walioko katika viunga vya magharibi na kusini mwa mkoa wa Halab (Aleppo) huko kaskazini mwa Syria wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya raia katika mji wa Halab, vijiji na vitongoji vya kandokando yake na kwamba hadi sasa idadi kubwa ya raia wameuawa na wengine kujeruhiwa.
Mauaji hayo ya makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Marekani, Saudi Arabia, Israel na waitifaki wao, yanafanyika sambamba na operesheni kubwa iliyoanzishwa na jeshi la taifa la Syria ya kukomboa kikamilifu maeneo yote ya kusini mashariki mwa mkoa wa Idlib na kandokando ya Halab.
Mkoa wa Idlib unatambuliwa kuwa ngome ya mwisho na makundi ya kigaidi nchini Syria na kukombolewa kwa mkoa huo, maeneo ya magharibi mwa Halab na mashariki mwa Latakia kutafunga kabisa virago vya magaidi nchini humo.