Algeria yataka Syria irejeshwe kwenye Jumuiya ya Nchi za Kiarabu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i59143-algeria_yataka_syria_irejeshwe_kwenye_jumuiya_ya_nchi_za_kiarabu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria ameziasa nchi za Kiarabu ziharakishe mchakato wa kuirejesha Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 14, 2020 04:04 UTC
  • Algeria yataka Syria irejeshwe kwenye Jumuiya ya Nchi za Kiarabu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria ameziasa nchi za Kiarabu ziharakishe mchakato wa kuirejesha Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League).

Sabri Boukadoum alisema hayo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, kukosekana Syria katika jumuiya hiyo ni pigo sio tu kwa jumuiya hiyo, bali kwa nchi zote za Kiarabu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria ameeleza bayana kuwa, kuna haja ya kuirejesha Syria katika jumuiya hiyo ya kikanda ili kuimarisha ushirikiano na umoja wa kieneo.

Mwishoni mwa mwaka 2018, Ahmed Aboul Gheit, Katibu Mkuu wa Arab League alinukuliwa na gazeti la Al Bayan la Imarati akisema kuwa, kwa mtazamo wake maamuzi ya kuiondoa Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu yalikuwa makosa makubwa.

Kikao cha Arab League mjini Cairo, Misri

Aidha mapema mwaka jana, Aboul Gheit alisema kuwa, licha ya kwamba suala la Syria ni tata kutokana na uingiliaji wa madola ya kigeni, lakini bila ya shaka yoyote Damascus itarejeshewa uanachama wake katika jumuiya hiyo.

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) kupitia mashinikizo mbalimbali ya nchi za Magharibi ilitangaza kusimamisha uanachama wa Syria katika jumuiya hiyo mwezi Novemba 2011, muda mfupi baada ya kuanza mgogoro wa ndani katika nchi hiyo ya Kiarabu.