Raia 30 wauawa Yemen katika mashambulizi mapya ya anga ya Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i59182-raia_30_wauawa_yemen_katika_mashambulizi_mapya_ya_anga_ya_saudia
Kwa akali raia 30 wameuawa katika wimbi jipya la mashambulizi ya anga ya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia katika mkoa wa Jawf, kaskazini mwa Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 16, 2020 03:28 UTC
  • Raia 30 wauawa Yemen katika mashambulizi mapya ya anga ya Saudia

Kwa akali raia 30 wameuawa katika wimbi jipya la mashambulizi ya anga ya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia katika mkoa wa Jawf, kaskazini mwa Yemen.

Kanali ya televisheni ya al-Masirah imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, muungano huo vamizi wa Saudia ulifanya mashambulizi manane ya anga jana Jumamosi katika wilaya ya al-Maslub mkoani Jawf, na kuua raia wasio na hatia.

Vyombo vya habari vya Yemen vimeripoti kuwa, baadhi ya mashambulizi hayo yalilenga raia wa Yemen waliokuwa wamekusanyika kutazama mabaki ya ndege ya kivita ya Saudia iliyotunguliwa na vikosi vya Yemen Ijumaa jioni katika mkoa wa Jawf.

Ndege ya kijeshi ya Saudia iliyotunguliwa mkoani Jawf na majeshi ya Yemen

Wizara ya Afya ya Yemen imeeleza kuwa, Saudi Arabia na washirika wake wameanzisha wimbi jipya la mashambulizi ya anga dhidi ya raia waliodhulumika wa Yemen na kwamba watoto na wanawake ni miongoni wma waliouawa katika shambulizi la jana.

Tangu Machi 2015 na kwa misaada na uungaji mkono wa Marekani, Saudia na Imarati zimeivamia kijeshi Yemen na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa anga, nchi kavu na baharini. Uvamizi na hujuma za kijeshi za Saudia na waitifaki wake, hadi sasa zimeshaua zaidi ya watu elfu 16, kujeruhi makumi ya melfu na kuwafanya mamilioni ya watu wapoteze makazi yao na kuwa wakimbizi.