Arab League yaunga mkono kurejeshwa Syria katika jumuiya hiyo
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) amekaribisha kurejeshwa Syria katika jumuiya hiyo.
Ahmed Aboul Gheit amesema, Algeria na nchi kadhaa za Kiarabu zinataka Syria kurejeshewa kiti chake ndani ya Arab League. Hii ni katika hali ambayo Jumamosi iliyopita Sabri Boukadoum, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria alikutana na Ahmed Aboul Gheit. Baada ya mkutano huo Boukadoum na Aboul Gheit walizungumza na waandishi wa habari ambapo katibu mkuu wa jumuuiya hiyo alisema, hadi sasa Arab League haijafahamu msimamo halisi wa Syria kuhusu kurejea kwake kwenye jumuiya hiyo, lakini Algeria na nchi kadhaa za Kiarabu zinataka kuiona ikirejea tena. Hivi karibuni pia Sabri Boukadoum, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria alinukuliwa akisema kuwa, nchi yake imeitaka Arab League kuirejesha Syria katika jumuiya hiyo.
Itakumbukwa kuwa kufuatia machafuko yaliyotokana na njama za madola ya Magharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu zikiongoza na Marekani na Saudi Arabia, jumuiya hiyo iliamua kusimamisha uanachama wa Syria kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali halali ya Rais Bashar al Assad. Licha ya upinzani mkubwa wa Saudia, lakini nchi nyingi za Kiarabu na kufuatia ushindi mtawalia wa serikali ya Damascus dhidi ya makundi ya kigaidi, zimekuwa zikiitaka Arab League kuirejeshea kiti chake Damascus ndani ya jumuiya hiyo.