Msimamo wa wanamgambo wa Taliban wa kutoitambua rasmi serikali ya Afghanistan
Mjumbe mwandamizi wa timu ya mazungumzo ya kundi la wanamgambo wa Taliban amesema kuwa, kundi hilo haliitambui rasmi serikali ya kutwishwa ya Afghanistan.
Sher Mohammad Abbas Stanakzai sambamba na kulaani himaya na uungaji mkono wa Marekani kwa serikali ya sasa ya Afghanistan chini ya uongozi wa Rais Ashraf Ghani amesema kuwa, wananchi wa nchi hiyo hawaridhishwi na serikali hiyo na wanaiona kuwa si serikali halali.
Mjumbe huyo mwandamizi wa timu ya mazungumzo ya kundi la wanamgambo wa Taliban ameongeza kuwa, baada ya kutiwa saini hati ya makubaliano ya amani baina ya wanamgambo hao na serikali ya Marekani, kundi hilo litafanya juhudi katika mazungumzo yake na makundi ya Kiafghani ili kupatikane serikali ambayo itaridhiwa na wananchi wote wa Afghanistan.
Matamshi ya Sher Mohammad Abbas Stanakzai, mjumbe mwandamizi wa timu ya mazungumzo ya kundi la wanamgambo wa Taliban kwamba, kundi hilo haliitambui serikali ya Afghanistan ni kukaririwa msimamo wa Taliban wa huko nyuma ambapo walimwengu walikuwa wakitaraji kwamba, baada ya kutiwa saini makubaliano ya amani kati yake na Marekani na kuandaliwa mazingira ya mazungumzo baina ya Waafghani, basi misimamo ya kundi hilo la wanamgambo ingebadilika.
Hatua ya wanamgambo wa Taliba ya kuendelea kusisitiza kwamba, hawaitambui serikali ya Afghanistan imeibua wasiwasi huu kwamba, kundi hilo licha ya kuingia katika duru mpya ya matukio ya nchi hiyo baada ya kutilitiana saini makubaliano ya amani na Marekani, lakini bado halijabadilisha muamala na utendaji wake.
Kutangazwa msimamo huo na Sher Mohammad Abbas Stanakzai, ambaye ni mjumbe wa ngazi za juu wa Taliban wa kutoitambua rasmi serikali ya sasa ya Kabul, kunaibua swali hili kwamba, mazungumzo baina ya Waafgghani ambayo yalipangwa kuanza kufanyika baada ya kufikiwa makubaliano ya kundi hilo na Marekani yatakuwa na hatima gani?
Misimamo iliyotangazwa na kundi la wanamgambo wa Taliban baada ya kufikiwa makubaliano ya amani kati yake na Marekani ambayo yanajumuisha ulazima wa kuachiliwa huru na serikali wafungwa wa kundi hilo kabla ya kuanza mazungumzo baina ya Waafghani na kadhalika kundi hilo kutoitambua serikali ya sasa ya nchi hiyo ni ishara ya wazi kwamba, kama ilivyotabiriwa utendaji wa Marekani katika kuandaa vipengee vya makubaliano hayo ulikuwa ni kuhakikisha kuwa, makubaliano hayo yanakwenda kinyume kabisa na matakwa pamoja maslahi ya taifa na mamlaka ya kujitawala Afghanistan.
Wasiwasi huu daima ulikuweko kabla ya kutiwa saini makubaliano ya amani ya Marekani na kundi la Taliban ambapo katika makubaliano haya inachofuatilia Washington ni njia ya kuondooka nchini Afghanistan bila ya kuzingatia udharura wa kutiwa vigezo na mitazamo ya serikali ya Kabul kama namna ya kuhitimishwa vita, kurejeshwa amani na kundi la Taliban kuikubali katiba ya nchi hiyo, ambapo misimamo ya hivi karibuni ya kundi hili inathibitisha kwamba, wasiwasi huo haukuwa bure bali ulikuwa na ukweli ndani yake.
Msimamo wa Sher Mohammad Abbas Stanakzai, mjumbe wa ngazi za juu wa Taliban katika mazungumzo wa kutoitambua rasmi serikali ya sasa ya Afghanistan unaipa nguvu dhana hii kwamba, kundi hilo linataka kuleta mabadiliko ya kimsingi katika muundo wa nchi hiyo ikiwemo katiba ili kwa njia hiyo liweze kuweka mitazamo yake katika muundo huo, hatua ambayo iko kinyume kabisa na matakwa ya uma nchini Afghanistan.
Inaonekana kuwa, baada ya kutangazwa msimamo huo na Sher Mohammad Abbas Stanakzai, sasa kufanyika mazungumzo baina ya Waafghani ni sarabi na mazigazi ambayo yameletwa na Marekani ambapo katika makubaliano na kundi la wanamgambo wa Taliban suala la kukubaliwa katiba na wanamgambo hao au hata kundi hilo kuitambua rasmi serikali ya Afghanistan na kukabidhiwa serikali ya Kabul suala la uamuzi wa kuwaachilia huru wafungwa wa Taliban ni mambo ambayo hayajatiwa na kujumuishwa katika makubaliano hayo ya amani.