Hashdu sh-Sha'abi ya Iraq: Tutalipiza kisasi mashambulizi ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i59781-hashdu_sh_sha'abi_ya_iraq_tutalipiza_kisasi_mashambulizi_ya_marekani
Moja ya makundi yanayounda Harakati ya Wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi nchini Iraq limesema kuwa, makundi ya muqawama ya Iraq yatalipiza kisasi dhidi ya mashambulizi ya Marekani na kwamba kisasi hicho kitakuwa cha kuumiza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 16, 2020 08:55 UTC
  • Hashdu sh-Sha'abi ya Iraq: Tutalipiza kisasi mashambulizi ya Marekani

Moja ya makundi yanayounda Harakati ya Wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi nchini Iraq limesema kuwa, makundi ya muqawama ya Iraq yatalipiza kisasi dhidi ya mashambulizi ya Marekani na kwamba kisasi hicho kitakuwa cha kuumiza.

Ali Al-Yasiri, Katibu Mkuu wa Muqawama wa 'Saraya Al-Khurasani' lenye mfungamano na Hashdu sh-Sha'abi ya Iraq ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya Al-Alam na kusisitiza kuwa mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani ndani ya ardhi ya Iraq, ni ukiukaji wa wazi wa haki ya kujitawala  nchi hiyo. Al-Yasiri amebainisha kuwa, woga wa jibu kali la makundi ya muqawama dhidi ya jinai za Marekani, umeukumba ubalozi wa Marekani nchini Iraq na kwamba hali hiyo itaendelea hadi wavamizi hao watakapoondoka Iraq.

Askari vamizi wa Marekani nchini Iraq

Itakumbukwa kuwa kambi ya kijeshi ya askari wa Marekani katika eneo la Al-Taji nchini Iraq, ilishambuliwa na makombora karibu 10 ya Katyusha ambapo askari wawili wa Marekani na mwingine wa Uingereza waliuawa huku wengine wakijeruhiwa. Licha ya harakati ya Hashdu sh-Sha'abi kusisitiza kutohusika kwa aina yoyote na shambulizi hilo, lakini Alkhamisi na Ijumaa iliyopita ndege za kivita za Marekani zilitekeleza mashambulizi dhidi ya maeneo ya harakati hiyo pamoja na ya jeshi la Iraq katika maeneo tofauti ya nchi hiyo ambapo watu kadhaa waliuawa na kujeruhiwa.