Kumalizika mzingiro wa Qatar, suluhu inayoyumbayumba
Makubaliano ya kukomeshwa mzingiro wa nchi kadhaa za Kiarabu dhidi ya Qatar yametiwa saini katika kikao cha al Ula nchini Saudi Arabia bila ya kuhudhuriwa na viongozi wa nchi za Imarati, Misri, Bahrain na Oman.
Mkutano wa 41 wa viongozi wa nchi za Kiarabu wanachama wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi (GCC) ulifanyika jana tarehe 5 Januari katika mji wa al Ula nchini Saudia. Lengo kuu la mkutano huo lilikuwa kukomesha mzingiro wa Qatar na kupatanisha baina ya nchi wanachama wa baraza hilo.
Mgogoro baina ya Qatar na nchi nne za Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri ulianza mwezi Juni mwaka 2017. Kutoridhishwa na siasa za nje za Qatar ndiyo sababu kuu ya kujitokeza mgogoro huo. Baada ya kukata uhusiano na Qatar, nchi hizo nne za Kiarabu ziliizingira nchi hiyo na kufunga mipaka yao na nchi hiyo. Baadaye ziliainisha Doha masharti 13 kwa ajili ya kufungua mipaka yao na Qatar na kuhuisha uhusiano na nchi hiyo. Miongoni mwa masharti hayo ni kufanya mabadiliko katika shughuli za televisheni ya al Jazeera, kukata uhusiano na harakati ya mapambano ya ukombozi wa Palestina ya Hamas na Ikhwanul Muslimin na vilevile kutazama upya uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kwa upande wake, Qatar ilikataa masharti hayo 13 na kutangaza kuwa yanapingana na mamlaka yake na haki ya kujitawala nchini hiyo. Sasa na baada ya kupita miaka mitatu na nusu, Saudi Arabia imefikia makubaliano ya kurejesha uhusiano na Qatar na kufungua mipaka yake na nchi hiyo licha ya kwamba Doha imekataa masharti hayo.
Nukta nyingine ya kutiliwa maanani ni kwamba, kikao cha al Ula kimefanyika chini ya upatanishi wa Kuwait na Marekani. Hapo kabla pia serikali ya Kuwait ilifanya juhudi za kupatanisha baina ya pande hizo mbili japokuwa hazikuzaa matunda. Inaonekana kuwa, kushindwa Donald Trump katika uchaguzi wa rais wa Marekani ni miongoni mwa sababu za kufanikiwa upatanishi wa sasa baina ya Saudia na Qatar. Katika siku za mwishoni mwa uhai wake, serikali ya Trump imechukua hatua ya kuhitimisha hitilafu na mzozo baina ya waitifaki hao wawili wa Marekani. Kushiriki kwa mshauri na mkwe wa Trump, Jared Kushner, katika kikao cha al Ula ni kielelezo cha ukweli huo. Mtaalamu wa masuala ya eneo la Magharibi mwa Asia, Qassem Muhibbu-Ali anasema: Mivutano baina ya Saudi Arabia na wenzake kwa upande mmoja na Qatar katika upande wa pili ilianza miezi kadhaa baada ya Donald Trump kuingia ikulu ya White House, na makubaliano ya kukomesha mivutano hiyo yamefikiwa katika siku za mwishoni za Trump ndani ya White House."
Wakati huo huo Saudi Arabia ina wasiwasi kwamba, kuja madarakani serikali ya Joe Biden nchini Marekani kutaimarisha mtazamo uliodhidi ya Riyadh mjini Washington. Kwa msingi huo Aal Saud wameamua kufumbia macho masharti yao 13 kwa serikali ya Qatar kwa shabaha ya kuhepa moja kati ya changamoto kubwa zaidi katika siku za usoni.
Nukta nyingine muhimu ni kwamba, mkutano wa al Ula haukuhudhuriwa isipokuwa na viongozi wa nchi mbili tu kati ya sita wa nchi wanachama wa GCC yaani viongozi wa Kuwait na Qatar. Mfalme Salman wa Saudia hakushiriki katika mkutano huo na aliwakilishwa na mwanaye, Muhammad bin Salman.
Japokuwa Misri si mwanachama katika Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi (GCC) lakini inahesabiwa kuwa katika kundi la mahasimu wa Qatar. Kiongozi wa nchi hiyo, Abdel Fattah al Sisi pia hakushiriki katika mkutano wa al Ula na badala yake amewakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Sameh Shoukry.
Kutoshiriki viongozi wa Bahrain, Imarati na Misri katika kikao cha al Ula ni ithibati kuwa Saudia imepatana na Qatar bila ridhaa ya nchi hizo tatu; na katika upande mwingine ni kwamba mapatano hayo hayakujengeka katika misingi imara na madhubuti.