Rais wa Iran: Jamhuri ya Kiislamu inapambana na vitendo vya kuhatarisha usalama na kuzusha machafuko katika eneo hili
(last modified 2024-10-04T02:26:02+00:00 )
Oct 04, 2024 02:26 UTC
  • Rais wa Iran: Jamhuri ya Kiislamu inapambana na vitendo vya kuhatarisha usalama na kuzusha machafuko katika eneo hili

Rais wa Iran amesisitiza kuwa, iwapo utawala wa Kizayuni utafanya kosa lolote la kijinai, basi utakumbwa na jibu madhubuti na kali na kwamba Jamhuri ya Kiislamu inapambana na vitendo vya utawala ghasibu wa Kizayuni vya kuzusha machafuko na kueneza mgogoro katika eneo hili.

Rais Masoud Pezeshkian jana Alhamisi alikuwa na mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na mwenyeji wake, Amir wa Qatar Sheikh Naim bin Hamad Aal Thani katika mji mkuu wa nchi hiyo Doha na alisisitiza kuwa  iwapo utawala wa Kizayuni utafanya kosa la kijinai, Jamhuri ya Kiislamu itatoa jibu kali na madhubuti kwa utawala huo. Amesema, kuzusha machafuko na kupanua mgogoro ni kati ya malengo maovu ya utawala wa Kizayuni katika eneo hili.

Rais Pezeshkian amesema: Iran inatilia maanani usalama wa ukanda huu umzima na inaamini kwamba ni sawa na usalama wake mwenyewe na wa Waislamu wote na ndio maana Tehran inataka kuona amani na ututulivu unadumishwa kwenye eneo hili hivyo ni utawala wa Kizayuni ndio ambao unafanya njama za kila namna za kuvuruga usalama wa ukanda huu.  

Rais wa Iran ameashiria kuuliwa shahid hapa Tehran mwanamuqawama Ismail Haniyeh, aliyekuwa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ambaye alikuwa mgeni rasmi wa Jamhuri ya Kiislamu na kusema: Nchi za Magharibi ziliiomba Iran eti isichukue hatua zozote za kujibu jinai hiyo kwa madai kuwa kungevuruga juhudi za kufikiwa haraka makubaliano ya kusitisha vita Ukanda wa Gaza lakini Wazayuni wameshadidisha hujuma zao za kikatili badala ya kusitisha jinai na mauaji yao ya kimbari na wanaishambulia pia Lebabon mbali na kufanya mashambulizi huko Gaza.

Rais Pezeshkian katika mkutano wa ACD mjini Doha, Qatar 

Pezeshkian amesisitiza kuwa viongozi wa Marekani na nchi za Magharibi wanapasa kuwalazimisha vibaraka wao katika eneo hili kuacha kufanya mauaji ya kimbari na jinai nyingine na kutoyumbisha usalama wa eneo hili kwa sababu ukosefu wa usalama si kwa maslahi ya mtu au serikali yoyote, bali ni hata kwa maslahi ya nchi za Ulaya na Marekani. 

Rais wa Iran aidha ameeleza kuwa Iran inakaribisha kuimarisha uhusiano na Qatar na kuongeza kuwa, nchi  hizi mbili zina nia moja ya kuimarisha ushirikiano kati yao. 

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran juzi Jumatano alielekea Doha, mji mkuu wa Qatar kwa madhumuni ya kushiriki katika Mkutano wa wakuu wa Jukwaa la Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia katika ziara yake ya siku mbili nchini humo.

Rais wa Iran alilakiwa na Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani.

Tags