Iran na Qatar zatiliana saini hati 6 za mikataba ya ushirikiano
(last modified Thu, 03 Oct 2024 04:22:53 GMT )
Oct 03, 2024 04:22 UTC
  • Iran na Qatar zatiliana saini hati 6 za mikataba ya ushirikiano

Maafisa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Qatar wamelitiana saini hati 6 za mikataba ya ushirikiano wa pamoja katika nyanja mbalimbali.

Utilianaji saini huo uliofanyika Doha Qatar, unahusisha sekta mbalimbali za kiuchumi na kibiashara, kiutamaduni, kielimu na michezo.

Ushirikiano katika mpango wa upanuzi wa Bandari ya Dayyer, sekta ya afya, ustawi na biashara mubashara, mpango wa utekelezaji wa ushirikiano wa kiutamaduni na mpango wa utekelezaji wa ushirikiano wa michezo hadi 2026 ni kati ya hati muhimu zaidi za ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, ambazo zilitiwa saini na mawaziri wa nishati, mambo ya nje na Michezo na vijana wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wenzao wa Qatar.

Rais Masoud Pezeshkian akiuongoza ujumbe wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana aliwasili Doha mji mkuu  wa Qatar na kulakiwa na Amir wa nchi hiyo Sheikh Tamim bin Hamad.

Hafla ya kumkaribisha rasmi nchini Qatar  Rais Masoud Pezeshkian 

 

Mbali na kukutana na kufanya mazungumzo ya pande mbili, Rais Pezeshkian atashiriki pamoja na Amir wa Qatar katka vikao vya ngazi ya juu vinavyohusu masuala ya nchi mbili.

Katika siku ya pili ya safari yake nchini Qatar Alkhamisi ya leo, Daktari Pezeshkian atashiriki na kutoa hotuba katika mkutano wa 19 wa Jukwaa la Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia (ACD) na pia atakuwa na mikutano na baadhi ya viongozi na maafisa wa nchi zinazoshiriki katika jukwaa hilo.

Jukwaa la Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia (ACD) ambalo lina nchi wanachama 22 ndilo kongamano kubwa zaidi la Asia ambalo lilianzishwa mwaka 2002 kwa lengo la kuendeleza ushirikiano wa kuitamaduni, kiuchumi na kijamii.