Qatar yakadhibisha madai ya kufunga ofisi ya HAMAS mjini Doha
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar amepuuzilia mbali ripoti za baadhi ya vyombo vya habari kuhusu kufungwa kwa ofisi ya Harakati ya Muqawamawa wa Kiislamu ya Palestina HAMAS mjini Doha.
Majed bin Mohammed al-Ansari, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar amekanusha vikali taarifa kuhusu kufungwa kwa ofisi ya tawi la kisiasa la Hamas mjini Doha.
"Habari kuhusu (kufungwa) ofisi ya Hamas huko Doha si za kweli," mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Qatar amesisitiza katika taarifa kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X.
Amesisitiza kuwa, lengo kuu la kuwepo kituo cha ofisi ya kisiasa ya Hamas huko Doha ni kudumisha "njia ya mawasiliano kati ya pande zinazohusika".
Mtandao wa habari wa lugha ya Kiebrania wa Kan awali ulikuwa umedai kuwa, Qatar imewaambia viongozi wa kisiasa wa Harakati ya HAMAS kwamba "hawatakiwi tena" katika nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi. Mtandao huo umedai, uamuzi huo wa serikali ya Doha umefikishwa kwa viongozi wa Hamas katika "siku za hivi karibuni".
Inadaiwa kuwa, baadhi ya maseneta wa chama cha Republican nchini Marekani wiki hii waliiandikia barua serikali ya Biden kuiomba ibadilishe sera yake kuhusiana na Qatar.