HAMAS yalitolea wito Baraza Kuu la PLO: Vunjeni uhusiano wenu wa kiusalama na Israel
(last modified Thu, 24 Apr 2025 04:13:13 GMT )
Apr 24, 2025 04:13 UTC
  • HAMAS yalitolea wito Baraza Kuu la PLO: Vunjeni uhusiano wenu wa kiusalama na Israel

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imelitaka Baraza Kuu la Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO livunje uhusiano wa uratibu wa kiusalama uliopo baina yake na utawala wa Kizayuni na kuchukua msimamo wa pamoja wa Palestina dhidi ya mauaji ya kinyama yanayoendelea huko Ghaza.

Hamas imesisitiza kuwa, kikao cha Baraza Kuu la Palestina au Baraza Kuu la PLO kinachofanyika huko Ramallah katika kipindi hiki kigumu kinaweza kutoa fursa mwafaka ya kuchukuliwa msimamo wa kitaifa na wa pamoja wa kukabiliana na mauaji ya kimbari yanayoendelea.
 
Hamas vilevile imewataka wajumbe wa Baraza Kuu la PLO kutimiza wajibu wao wa kitaifa na kukataa usimamizi wa kutwishwa wa maisha ya kisiasa ya Wapalestina, na kuchukua uamuzi madhubuti kwa lengo la kuiamilisha Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO), kuijenga upya kwa msingi wa ushirikishaji na kutekeleza jukumu lake halisi, sambamba na kufuatilia kesi za kisheria katika mahakama za kimataifa dhidi ya wazayuni maghasibu kutokana na jinai walizofanya.
 
Hamas imetangaza kuwa mkutano huo ambao unafanyika baada ya kupita mwaka mmoja na nusu wa vita dhidi ya Ghaza tena bila ya kukamilishwa taratibu zake, hauhesabiki kuwa ni mjumuiko kamili wa kitaifa na wala haujumuishi wahusika wote wa jamii ya Palestina.
 
Harakati ya Hamas imesisitiza kuwa mkutano huo unapaswa utilie maanani kiwango cha kujitolea mhanga kilichoonyeshwa na wananchi wa Palestina na kupitisha maamuzi ya kiuwajibikaji kwa ajili ya kukomesha vita.
 
Halikadhalika, harakati hiyo ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina imetoa wito wa kutekelezwa maazimio ya huko nyuma ya Baraza Kuu, muhimu zaidi likiwa ni kusitishwa uratibu wa kiusalama, kuvunjwa uhusiano na utawala wa Kizayuni, na kuzidishwa Muqawama dhidi ya maghasibu na miradi yao ya Uyahudishaji na ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi, ambayo inalenga kuugawanya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kufuta mamlaka ya utawala ya Palestina.../