Qatar: Mapatano na Saudia hayabadilishi uhusiano wetu na Iran
(last modified Fri, 08 Jan 2021 02:39:40 GMT )
Jan 08, 2021 02:39 UTC
  • Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Aal-Thani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar
    Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Aal-Thani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar

Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar amesema mapatano ya nchi yake na Saudia Arabia pamoja na waitifaki wake hayatabadilisha uhusiano mzuri ulioko baina ya Qatar na nchi zingine ikiwemo Iran.

Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Aal-Thani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar ameyasema hayo Alhamisi katika mahojiano na gazeti la Financial Times la Uingereza na kuongeza kuwa: "Uhusiano wa pande mbili wa Qatar na nchi zingine umejengeka katika msingi wa maamuzi huru na kwa mujibu wa maslahi ya kitaifa."

Aal-Thani ameongeza kuwa, muda mrefu umechukuliwa kabla ya kurejeshwa uhusiano wa kirafiki baina ya Qatar na baadhi ya nchi za Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi na kuongezxa kuwa nchi yake inataka matatizo ya kieneo yatatuliwe.

Makubaliano ya kukomeshwa mzingiro wa nchi kadhaa za Kiarabu dhidi ya Qatar yalitiwa saini katika kikao cha al Ula nchini Saudi Arabia.

Mkutano wa 41 wa viongozi wa nchi za Kiarabu wanachama wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi  ulifanyika tarehe 5 Januari katika mji wa al Ula nchini Saudia. Lengo kuu la mkutano huo lilikuwa kukomesha mzingiro wa Qatar na kupatanisha baina ya nchi wanachama wa baraza hilo.

Mgogoro baina ya Qatar na nchi nne za Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri ulianza mwezi Juni mwaka 2017. Kutoridhishwa na siasa za nje za Qatar ndiyo sababu kuu ya kujitokeza mgogoro huo. Baada ya kukata uhusiano na Qatar, nchi hizo nne za Kiarabu ziliizingira nchi hiyo na kufunga mipaka yao na nchi hiyo. Baadaye ziliainisha Doha masharti 13 kwa ajili ya kufungua mipaka yao na Qatar na kuhuisha uhusiano na nchi hiyo. Miongoni mwa masharti hayo ni kufanya mabadiliko katika  shughuli za televisheni ya al Jazeera, kukata uhusiano na harakati ya mapambano ya ukombozi wa Palestina ya Hamas na Ikhwanul Muslimin na vilevile kutazama upya uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwa upande wake, Qatar ilikataa masharti hayo 13 na kutangaza kuwa yanapingana na mamlaka yake na haki ya kujitawala nchini hiyo. 

Tags