Makubaliano ya AI-Ula Saudi Arabia na engo zake tofauti
(last modified Sat, 09 Jan 2021 02:39:39 GMT )
Jan 09, 2021 02:39 UTC
  • Makubaliano ya AI-Ula Saudi Arabia na engo zake tofauti

Kikao cha Baraza na Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi kilifanyika Jumanne iliyopita ya tarehe 5 Januari katika mji wa Al-Ula Saudi Arabia na kuhitimishwa mzingiro dhidi ya Qatar uliodumu kwa zaidi ya miaka mitatu.

Hakuna taarifa zenye kutoa maelezo ya kina kuhusiana na mapatano hayo. Hata hivyo kuna tathmini mbalimbali zinazotolewa na weledi wa mambo kuhusiana na makubaliano hayo.

Mosi; Saudia ikiwa na lengo la kufikia makublaiano na Qatar imezipuuza nchi nyingine tatu za Bahrain, Imarati na Misri ambazo zilikuwa pamoja nayo katika mzingiro na mashinikizo dhidi ya Qatar. Ndio maana hata katika mkutano huo wa Al-Ula hakuna nchi yoyote kati ya hizo tatu ambayo ilituma mwakilishi wa ngazi za juu katika mkutano huo. Hii ni ishara tosha kwamba, mzozo wa Qatar bado ungalipo na hadi sasa katika Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi kungali kuna kambi kadhaa.

Pili; Imarati ndio iliyopata pigo kubwa kufuatia makubaliano ya Al-Ula. Katika miezi ya hivi karibuni Imarati imekuwa na mzozo katika uhusiano wake na Uturuki, katika hali ambayo uhusiano wa Qatar na Ankara umeboreka na kustawi mno. Katika upande mwingine Imarati imekuwa ikidai kwamba, ndio nchi muhimu yenye taathira katika matukio ya eneo la Asia Magharibi ukiwemo ulimwengu wa Kiarabu. Hata hivyo hatua ya Saudia ya kufikia makubaliano na Qatar katika mkutano wa Al-Ula kivitendo imeipuuza Imarati. Ni kwa msingi huo, ndio maana Muhammad bin Zayed al-Nahyan, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Abu Dhabi hakushiriki katika mkutano huo, hatua ambayo ni ujumbe wazi kwamba, hakuridhishwa na mwenendo huo wa Riyadh.

Hatimaye baada ya miaka mitatu na nusu, mzingiro dhidi ya Qatar umehitimishwa baada ya Saudia kutiliana saini na Doha

 

Tatu; makubaliano ya Al-Ula, yamedhihirisha kufanikiwa Qatar katika kusimama kwake kidete mkabala wa mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa ya Saudia na mataifa mengine matatu ya Kiarabu. Katika kipindi cha miaka mitatu na nusu iliyopita, Saudi Arabia ikishirikiana na Bahrain, Misri na Imarati zilitumia wenzo wa mzingiro na vikwazo ili kuishinikiza Qatar ibadilishe siasa zake za kigeni. Hata hivyo, serikali ya Doha ilisimama kidete na kusisitiza mara kadhaa kwamba, katu haiko tayari kusalimu amri kwani kufanya hivyo ni kukiuka mamlaka yake ya kujitawala. Qatar ilikataa katakata kukubali hata sharti moja kati ya masharti 13 iliyopatiwa na ikashiriki katika kikao cha Al-Ula.

Katika fremu hiyo, Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliandika katika ukurasa wake wa twitter Jumanne iliyopita baada ya kufikiwa makubaliano hayo kwamba: Pongezi kwa Qatar kwa kupata mafanikio baada ya kusimama kishujaa mbele ya mashinikizo, unyang’anyi na utumiaji mabavu.

 

Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Nne; makubaliano ya al-Ula ni ishara ya kufikia tamati nidhamu ya ubabe na utwishaji mambo ya fikra za ki-Trump dhidi ya eneo la Asia Magharibi. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Trump alifanya kila awezalo kulitwisha eneo la Asia Magharibi mfumo au nidhamu ya serikali huria au mfumo usio na sheria, Anarchical kwa kimombo. Katika aina hii ya mfumo, Marekani inakaribisha kwa mikono miwili fujo, vurugu na machafuko, inapinga amani na uthabiti kwani haviendani na maslahi yake; na inafuatilia maslahi na malengo yake kupitia kuendelea hali hii.

Kwa muktadha huo, licha ya kuwa, Saudia na Qatar wote ni washirika wa Marekani, lakini serikali ya Trump haijafanya juhudi zozote za kuhitimisha hitilafu na mzozo baina ya nchi hizo. Saudia nayo imetumia vyema utendaji huu wa Trump kwa ajili ya kutekeleza mantiki ya mabavu na ubabe katika siasa zake za nje dhidi ya nchi za eneo ikiwemo Qatar.

Mkutano wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi uliofanyika hivi karibuni katika mji wa al-Ula nchini Saudi Arabia

 

Tano; makubaliano ya Al-Ula hata kama ni ya kuyumbayumba na yamefanyika chini ya mashinikizo, lakini ni hatua nzuri na chanya kwa ajili ya nidhamu ya usalama Asia Magharibi. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, eneo la Asia Magharibi limepitia kipindi kigumu cha ukosefu wa usalama na uthabiti. Kwa msingi huo, kila makubaliano ambayo yanapelekea kupunguza mzozo na ukosefu wa usalama, bila shaka ni hatua yenye maslahi kwa nchi zote za eneo.

Hivyo basi, makubaliano haya yanaweza kuwa hatua moja mbele kwa ajili ya mazungumzo baina ya nchi za eneo kwa minajili ya kuhitimisha mivutano na chuki baina ya pande mbili na wakati huo huo kuimarisha amani na uthabiti wa eneo. Ni kwa msingi huo, ndio maana Muhammad Javad Zarif akazihutubu baadhi ya nchi za Kiarabu hususan Saudi Arabia kwa kuziambia: Umewadia wakati wa nyinyi kukubali pendekezo letu linalotaka kuweko eneo lenye nguvu.

Tags