Palestina yataka dunia iishinikize Israel iruhusu uchaguzi Quds
(last modified Thu, 29 Apr 2021 02:28:58 GMT )
Apr 29, 2021 02:28 UTC
  • Palestina yataka dunia iishinikize Israel iruhusu uchaguzi Quds

Msemaji wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameiasa jamii ya kimataifa iushinikize zaidi utawala wa Kizayuni wa Israel ili ukubali kufanyika uchaguzi wa Bunge la Palestina katika mji wa Quds (Jerusalem).

Nabil Abu Rudeineh amesema viongozi wa Palestina wanatazamiwa kukutana leo Alkhamisi ili kutangaza msimamo mmoja juu ya uchaguzi huo wa Bunge ambao unasubiriwa kwa hamu.

Amesema hadi sasa utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unajaribu kuvuruga mchakato wa uchaguzi huo umekataa kuwaruhusu waangalizi wa uchaguzi wa Ulaya kwenda kufuatilia zoezi hilo.

Ameeleza bayana kuwa, jamii ya kimataifa ina wajibu wa kuhakikisha kuwa vizuizi vyote vya kufanyika uchaguzi huo hususan katika mji wa Baitul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel vinaondolewa.

Msemaji wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesisitiza kuwa, msimamo wa Wapalestina uko wazi kwamba, hakuna uchaguzi utaofanyika iwapo mji wa Quds tukufu hautajumuishwa katika zoezi hilo la mwezi ujao.

Hamas inatazamiwa kung'ara katika uchaguzi ujao wa Bunge kama ilivyofanya 2006

Makundi ya muqawama bali hata makundi mengine ya kisiasa nchini Palestina yametahadharisha juu ya kutofanyika uchaguzi wa bunge mjini Quds na yameuonya vikali utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusu njama zake za kuvuruga uchaguzi huo.

Uchaguzi wa  Bunge la Palestina unatazamiwa kufanyika Mei 22 katika Ukingo wa Magharibi, Quds inayokaliwa kwa mabavu na Ukanda wa Gaza. Huu utakuwa uchaguzi wa kwanza kufanyika tangu miaka 14 iliyopita kwa lengo la kuwachagua wabunge Wapalestina.