Sep 19, 2021 16:33 UTC
  • Saudia kuwanyonga wafungwa 41, jumuiya za kimataifa zapaza sauti kupinga

Wafungwa 41 wanaoshikiliwa katika jela za Saudi Arabia wamehukumiwa kifo baada ya mahakama za nchi hiyo kutoa hukumu za kidhalimu dhidi ya wafungwa hao.

Mtandao wa Saudi Leaks umeripoti kuwa jumuiya za kutetea haki za binadamu zimefichua kwamba, tangu mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu maafisa wa serikali ya Saudi Arabia wametekeleza hukumu ya kifo dhidi ya mahabusu 50 na kwamba wafungwa wengine 41 wanakabiliwa na adhabu ya kifo. 

Ripoti ya Saudi Leaks imeongeza kuwa, mahakama za Saudia zimekuwa zikitoa hukumu za kifo za kidhalimu dhidi ya wafungwa na mahabusu bila ya kuwepo uwazi wala uadilifu bali kwa kuzingatia matamshi ya watuhumiwa waliolazimishwa kukiri makosa baada ya kuteswa na kunyanyaswa.

Ripoti hiyo imesema kuwa, maafisa wa serikali ya Saudi Arabia wanaendelea kutekeleza hukumu ya kifo dhidi ya mahabusu na wafungwa na kwamba mwaka 2019 pekee waliwanyonga wafungwa 184. 

Image Caption
Maelfu ya wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu wanasota jela Saudia

Wakati huo huo jumuiya ya kutetea haki za binadamu na Sanad imeitaka serikali ya Riyadh kuheshimu haki za binadamu na wafungwa. Vilevile imeitaka Saudia kuwaachia huru wafungwa ambao vifungo vyao vimemalizika.

Mwezi uliopita wa Agosti shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilitoa ripoti ambayo kwa mara nyingine tena imeweka wazi rekodi mbaya na nyeusi ya utawala wa Saudi Arabia katika suala la haki za binadamu.

Amnesty International ilitangaza kuwa, Saudi Arabia imezidisha ukandamizaji na kuwatesa wanaharakati wa kupigania haki za binadamu na haki za kiraia na kwamba idadi ya watu walionyongwa nchini humo pia imeongezeka sana katika kipindi cha miezi sita iliyopita. 

Tangu tarehe 21 Juni mwaka 2017 wakati Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud wa Saudia alipomteua mwanaye, Muhammad, kuwa mrithi mpya wa kiti cha ufalme katika kile kilichotambuliwa kuwa ni mapinduzi baridi dhidi ya ndugu yake, nchi hiyo ilikumbwa na wimbi kubwa la ukatili, ukandamizaji na kunyongwa wapinzani na watetezi wa haki za kiraia.  

Tags