Israel imewaua shahidi Wapalestina 17 katika mwezi huu wa Aprili
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i82526-israel_imewaua_shahidi_wapalestina_17_katika_mwezi_huu_wa_aprili
Utawala haramu wa Israel umeshadidisha mashambulizi yake dhidi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan tokea mwanzo wa mwezi huu wa Aprili kwa lengo la kuzima oparesheni za wananchi wanamapambano wa Palestina ambao wanakabiliana na jinai za utawala huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 15, 2022 03:13 UTC
  • Israel imewaua shahidi Wapalestina 17 katika mwezi huu wa Aprili

Utawala haramu wa Israel umeshadidisha mashambulizi yake dhidi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan tokea mwanzo wa mwezi huu wa Aprili kwa lengo la kuzima oparesheni za wananchi wanamapambano wa Palestina ambao wanakabiliana na jinai za utawala huo.

Miji ya Ukingo wa Magharibi hasa Jenin tokea mwanzo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani imeshuhudia kushadidi hujuma za utawala wa Kizayuni wa Israel ambapo hadi sasa idadi kubwa ya Wapalestina wameuawa shahidi na wengine kujeruhiwa baada ya kufyatuliwa risasi na askari wa utawala wa Kizayuni.

Alhamisi ya jana pia makumi ya vijana Wapalestina katika kitongoji cha Bitaa kusini mwa mji wa Nablus walipambana na askari wa utawala wa Kizayuni ambapo Wapalestina 35 walijeruhiwa.

Kwa mujibu wa tovuti ya Kipalestina ya Felestin Al Youm, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa utawala wa Israel tokea Aprili mwaka huu wa 2022 katika Ukingo wa Magharibi imefika 17.

Hali ndani ya Msikiti wa Al Aqsa baada ya askari wa utawala wa Israel kuuvamia mapema Ijumaa Aprili 15 2022

 

Wakati huo huo wanajeshi wa utawala haramu wa Israel mapema leo wameuvamia Msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem) na kuwajeruhi waumini Wapalestina ikiwa ni katika muendelezo wa uchokozi unaotekelezwa na utawala huo dhidi ya Wapalestina katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Shirika la Habari la Ma'an la Palestina limesema askari wa Israel waliuvamia Msikiti wa Al Aqsa mapema leo alfajiri kupitia lango la Al Mughrabi ambapo waliwafyatulia risasi za plastiki waumini waliokuwa msikitini.

Aidha wanajeshi hao wa Israel waliwashambulia wafanyakazi wa ambulensi ambao walifika msikitini hapo kuwasaidia majeruhi. Hilali Nyekundu ya Palestina imeripoti kuwa Wapalestina 90 wamekimbizwa hospitalini kupata matibabu baada ya kujeruhiwa katika hujuma hiyo ya Wazayuni.

Utawala wa Kizayuni wa Israel umezidisha jinai zake dhidi ya Wapalestina katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani na sasa Wapalestina nao wameimarisha harakati zao za mapambano ya kukabiliana na utawala huo dhalimu.