Syria yatungua makombora ya Israel nje ya Damascus
Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Syria kimetangaza kutungua makombora yaliyokuwa yamevurumishwa na ndege za utawala haramu wa Israel nje ya mji mkuu Damascus.
Shirika rasmi la habari la Syria, SANA limetangaza kuwa Alhamisi usiku mizinga ya ulinzi wa anga ya Syria ilitungua makombora hayo ya Israel ambayo yalikuwa yamevurumishwa kutoka Milima ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na utawala wa Israel.
Jeshi la utawala dhalimu wa Israel limekuwa likivurumisha makombora mara kwa mara nchini Syria lakini makombora mengi hutunguliwa na vikosi vya ulinzi wa anga vya nchi hiyo ya Kiarabu.
Mara kwa mara, Syria imekuwa ikilaani mashambulio ya utawala wa Israeli katika ardhi yake ikisema vitendo hivyo vya uchokozi vya Tel Aviv havitaathiri azma ya nchi hiyo ya Kiarabu katika vita dhidi ya ugaidi.
Lebanon pia hivi karibuni iliwasilisha mashtaka kwa Umoja wa Mataifa ikilalamikia hatua ya utawala haramu wa Israel kukiuka anga yake mara kwa mara wakati wa kutekeleza mashambulizi dhidi ya Syria.
Utawala haramu wa Israel ni muungaji mkono mkubwa wa magaidi ambao wanataka kuiangusha serikali halali ya Rais Bashar al Assad nchini Syria.