Haniyeh: Wapalestina kamwe hawatasalimu amri kwa Wazayuni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i82616-haniyeh_wapalestina_kamwe_hawatasalimu_amri_kwa_wazayuni
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesisitiza kuwa, Wapalestina kamwe hawatasalimu amri mbele ya jinai na vitendo vya kigaidi vya Wazayuni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 17, 2022 09:10 UTC
  • Ismail Haniyeh
    Ismail Haniyeh

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesisitiza kuwa, Wapalestina kamwe hawatasalimu amri mbele ya jinai na vitendo vya kigaidi vya Wazayuni.

Huku hali ya wasiwasi ikiendelea kutanda mjini Quds, leo (Jumapili) Msikiti wa Al-Aqsa umeshambuliwa tena na mamia ya wanajeshi wa Israel wakishirikiana na walowezi  wa Kizayuni, wanaojaribu kuwatimua waumini wa Kiislamu walioko katika eneo hilo kwa ajili ya ibada.

Habari za hivi karibuni zinasema kwamba, Wazayuni wanatumia mabomu ya sauti kuwafukuza Waislamu wa Kipalestina walioko ndani ya Msikiti wa Al-Aqsa. Watu walioshuhudia wanasema wanajeshi wa Israel wanawashambulia Wapalestina hao na kuwanyanyasa. 

Itakumbukwa kuwa, siku ya Ijumaa alfajiri, askari wa utawala haramu wa Israel waliwashambulia Wapalestina ndani ya Msikiti wa Al Aqsa mjini Quds (Jerusalem) ambapo zaidi ya waumini 160 wamejeruhiwa. Wapalestina wengine wasiopungua 400 wametiwa nguvuni. Jinai hiyo imewapa Wapalestina irada na azma kubwa zaidi ya kuimarisha mapambano yao dhidi ya adui Mzayuni mtenda jinai.

Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas amesema: Msikiti wa Al-Aqsa ni mali ya Waislamu, na Wayahudi hawana haki kabisa katika eneo hilo. Haniyeh ameongeza kuwa, ni haki ya Waislamu kuingia katika Msikiti wa Al-Aqswa, kuswali na kufanya itikafu, na kwamba Wapalestina kamwe hawatasalimu amri mbele ya vitendo vya kikatili na vya kigaidi vya Wazayuni.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas amesema, watu wa Palestina wanajilinda wao wenyewe na ardhi yao, na kwamba ni haki yao kuendelea na mapambano.

Hujuma ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Quds na Msikiti wa Al-Aqsa inafanyika licha ya kwamba, mwaka 2016 Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) lilipitisha azimio likipinga madai ya kuwepo uhusiano wa aina yoyote wa kihistoria, kidini au kiutamaduni baina ya Mayahudi maeneo matakatifu Quds haswa Msikiti wa Al-Aqsa, na kuutaja msikiti huo kuwa ni eneo takatifu kwa Waislamu.

Mji wa Quds, wenye Msikiti wa Al-Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu, ni sehemu muhimu ya Palestina na moja kati ya maeneo matakaifu sana ya Kiislamu.