Watoto zaidi ya elfu mbili Kipalestina wauliwa shahidi na Wazayuni
Wanajeshi katili wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamewauwa shahidi kwa kuwapiga risasi watoto wa Kipalestina zaidi ya elfu mbili tangu kuanza Intifadha ya Masjidul Aqsa mwaka 2000.
Wizara ya Habari ya Palestina imetangaza katika ripoti yake ya leo Jumatano kuwa tangu kuanza Intifadha ya Masjidul Aqsa mwaka 2000 hadi sasa, watoto wa Kipalestina 2079 wameshauliwa shahidi na wanajeshi wa Kizayuni huku wengine 1300 wakijeruhiwa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, utawala wa Kizayuni vile vile umeshawateka nyara watoto wa Kipalestina elfu 12 katika kipindi hicho, ambapo watoto 42 kati yao hadi sasa wamefungwa katika jela za utawala huo katili.
Wakati huo huo asilimia 95 ya watoto hao waliteswa vikali na kutendewa miamala mobovu na wanajeshi wa Israel wakati wa kutiwa nguvuni. Ripoti ya Wizara ya Habari ya Palestina imeongeza kuwa, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni kila mwaka huwateka nyara watoto 700 katika maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kwa visingizo visivyo na msingi. Intifadha ya Pili ya Wapalestina ilipamba moto tarehe 28 mwezi Disemba mwaka 2000 baada ya Ariel Sharon Waziri Mkuu wa wakati huo wa utawala wa Israel kuingia katika msikiti mtakatifu wa al Aqsa akiwa pamoja na wanajeshi kadhaa wa utawala huo pandikizi. Intifadha ya Kwanza ya Palestina au kwa jina jingingine Intifadha ya Mawe dhidi ya utawala wa Kizayuni ilianza mwezi Disemba mwaka 1978. Hii ni katika hali ambayo Intifadha Mpya ya Palestina yaani Intifadha ya Quds ilianza mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka jana kufuatia siasa za kichokozi na ukandamizaji zinazofanywa na utawala wa Kizayuni sambamba na njama zake za kutaka kubadili utambulisho wa Baitul Muqaddas na mpango wake wa kutaka kuugawa msikiti wa al Aqsa kwa mujibu wa wakati na kieneo. Wapalestina 250 wameuliwa shahidi hadi sasa katika Intifadha hiyo.