Muqtada Sadr aitaka Saudi Arabia ichukue mkondo wa siasa za wastani
Muqtada Sadr, Kiongozi wa Harakati ya Sadr ya nchini Iraq ameitolea wito Saudi Arabia na kuitaka ichukue mkondo wa siasa za kati na kati.
Muqtada Sadr amesema, endapo Muhammad bin Salman, mrithi kijana wa kiti cha ufalme wa Saudia atachuchukua mkondo wa siasa za wastani, hatua yake hiyo inaweza kuandaa mazingira ya kuleta umoja katika safu za Waislamu.
Ripoti iliyotolewa na Baghdad al-Yaum imemnukuu Sayyid Muqtada al-Sadr akisema kuwa, tuna matarajio kwamba, baada ya Misri kuukarabati msikiti wa Raas al-Hussein (as), serikali ya Saudi Arabia nayo itachukua hatua ya kuyakarabati makaburi ya Baqii mjini Madina.
Katika makaburi ya Baqii yaliyoko mjini Madina, kumezikwa watu wengi mashuhuri wa nyumba tukufu ya Bwana Mtume (saw) na masahaba wa Bwana Mtume wakiwemo Maimamu wanne wa Waislamu wa Mashia yaani Maimamu Hassan, Sajjad, Baqir na Swadiq (as).
Katika upande mwingine, Waislamu wa madhehebu ya Shia mashariki mwa Saudia wamekuwa wakijitokeza mara kwa mara na kufanya maandamano wakilalamikia ukandamizaji unaofanywa dhidi ya jamii yao na vikosi vya usalama vya utawala wa kifalme wa Saudia.
Mji wa Qatif wa mashariki mwa Saudia umekuwa ukishambuliwa mara kwa mara na wanajeshi wa Saudi Arabia na hadi sasa mamia ya wakazi wa mji huo wameuawa na wengine wengi kukamatwa kutokana na harakati zao za kisiasa sambamba na kubomoa misikiti na vituo vyao vya kidini.
Eneo hilo la mashariki mwa Saudia ndilo lenye utajiri mkubwa zaidi wa mafuta nchini humo lakini wakazi wa eneo hilo, ambao aghalabu ni Waislamu wa madhehebu ya Shia, wamekuwa wakikandamizwa na kudhulumiwa kwa muda mrefu sana.