Mkuwaiti mcheza shataranji akataa kuchuana na Muisraeli
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i83288-mkuwaiti_mcheza_shataranji_akataa_kuchuana_na_muisraeli
Raia wa Kuwait mcheza shataranji amekataa kuchuana na Muisraeli katika Mashindano ya Kimataifa ya Sunway ya Ubingwa wa Shataranji nchini Uhispania.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 05, 2022 05:48 UTC
  • Mkuwaiti mcheza  shataranji akataa kuchuana na Muisraeli

Raia wa Kuwait mcheza shataranji amekataa kuchuana na Muisraeli katika Mashindano ya Kimataifa ya Sunway ya Ubingwa wa Shataranji nchini Uhispania.

Hatua hiyo imechukuliwa kama njia ya kubainisha kufungamana na watu wa Palestina na ni pigo kwa utawala wa Kizayuni wa Israel unaokalia kwa mabavu ardhi za Palestina ambao unatafuta itibari kupitia michezo ya kimataifa.

Bader al-Hajri ni mmoja kati ya mabingwa wa shataranji nchini Kuwait na alikuwa mshindi wa mashindano ya San Sebastian ya Uhispania mwaka 2015.

Kufuatia uamuzi huo wa kishujaa wa al Hajri, wanaharakati Waarabu katika mitandao ya kijamii wamempongeza na kumtaja kuwa bingwa kwa kukataa sera za tawala za Kiarabu ambazo zimeanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel. Aidha wanaharakati wamesifu kitendo chake cha kukataa kuchuana na 'mlowezi Muisraeli' na kusema yeye ni fahari kwa Waarabu.

Mcheza vitara wa Kuwait Mohamed al-Fadli

Hii si mara ya kwanza kwa mwanamichezo wa Kuwait kukataa kucheza na Muisraeli. Mwezi uliopita mchezaji wa  vitara (fencing) kutoka Kuwait, Mohamed Al Fadli alijiondoa katika mashindano ya Ubingwa wa Kimataifa wa Vitara katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ili kujizuia kukutana na Muisraeli.

Aidha mapema mwaka huu, mchezaji maarufu wa mchezo wa tenisi kutoka Kuwait, Muhammad Al Awadi alijiondoa katika Mashindano ya J4  UAE mjini Dubai ambayo yalifanyika huko Imarati kuanzia Januari 17 hadi 22, ili asikutane na Mzayuni.

Katika miaka ya hivi karibuni wanamichezo kadhaa wa nchi za Kiislamu hasa Iran, Sudan, Libya, Algeria na Lebanon wamekataa kushiriki katika michuano na wanamichezo wa utawala haramu wa Israel.