Saudia ni katika nchi zinazoongoza kwa kukandamiza uhuru wa vyombo habari
Jumuiya ya Maripota Wasio na Mipaka imeitaja Saudi Arabia kuwa miongoni mwa nchi zinazofanya vbaya sana kwa upande wa uhuru wa vyombo vya habari.
Saudi Arabia ni moja ya nchi duniani inayowafunga jela waandishi wa habari kwa tuhuma kama kufanya njama dhidi ya utawala wa kifalme wa nchi hiyo na kushirikiana na taasisi za kigeni; huku ufuatiliaji wa kimahakama wa watuhumiwa hao ukiendelea kuwa kitendawili kikubwa.
Viongozi wa Saudi Arabia wameunda taasisi moja ya kuwafuatilia na kuwapeleleza waandishi wa habari na hivyo kukanyaga uhuru wa vyombo vya habari huku wakiwafunga jela watakavyo waandishi hao
Saudi Arabia ni miongoni mwa nchi tano za kwanza iliyo na waandishi habari wengi walioko korokoroni hadi kufikia Disemba Mosi mwaka jana. Hii ni kwa sababu, utawala wa Aal Saud umewatia nguvuni waandishi habari wasiopungua 31 tokea kuanza kampeni ya kuwatia mbaroni kilohela waandishi wa habari nchini humo.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa, kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari maripota wasio na mipaka wameitaja Saudi Arabia kuwa ni "jela mbaya zaidi kwa waandishi wa habari duniani".
Viongozi wa Saudia hawaaishii tu kuwatia mbaroni waandishi wa habari; bali utawala huo wa kifalme huwatesa aghalabu ya waandishi hao na hata kuwauwa. Mwandishi habari mashuhuri sana kati yao ni Jamal Khashoggi aliyekuwa akiukosoa utawala huo ambaye aliuliwa kinyama na Saudi Arabia akiwa ndani ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul Uturuki kwa kukosoa hali ya mambo ya Saudia.