Mkuu wa Baraza la Mamufti Russia atangaza kuunga mkono Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i83358-mkuu_wa_baraza_la_mamufti_russia_atangaza_kuunga_mkono_palestina
Mkuu wa Baraza la Mamufti nchini Russia ametangaza uungaji mkono wake wa taifa madhulumu la Palestina ambalo linakabailiwa na hujuma za kila upande za utawala haramu wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 07, 2022 06:43 UTC
  • Mkuu wa Baraza la Mamufti Russia atangaza kuunga mkono Palestina

Mkuu wa Baraza la Mamufti nchini Russia ametangaza uungaji mkono wake wa taifa madhulumu la Palestina ambalo linakabailiwa na hujuma za kila upande za utawala haramu wa Israel.

Sheikh Ravil Ainuddin ametangaza himaya na uungaji mkono wake huo katika mazungumzo yake mjini Moscow na Moussa Abu Marzouq, mjumbe mwandamizi wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiisamu ya Palestina HAMAS.

Sheikh Ravil Ainuddin amesisitiza katika mazungumzo hayo juu ya himaya na uungaji mkono wa Waislamu wa Russia kwa wananchi wa Palestina na kubainisha kwamba, hali ya mambo kwa Wapalestina huko Quds imekuwa ngumu na kwamba, anafuatilia kwa karibu yale yanayojiri katika mji huo mtakatifu.

Mkuu wa Baraza la Mamufti Russia sambamba na kuonyesha kuwa pamoja na Wapalestina walioko Baytul-Muqaddas amesema kuwa, kama kutakuweko na uwezekano basi yuko tayari kutoa msaada wa aina yoyote.

Sheikh Ravil Ainuddin, Mkuu wa Baraza la Mamufti Russia katika mazungumzo yake na ujumbe wa Hamas

 

Kadhalika kiongozi huyo wa kidini ameashiria juhudi za kidiplomasia za Russia kwa ajili ya kuipatia ufumbuzi kadhia ya Palestina na kueleza kwamba, Russia  inatambua rasmi azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotilia mkazo juu ya kuundwa dola huru la Palestina lengo mamlaka kamili.

Kwa upande wake, Moussa Abu Marzouq, afisa mwandamizi wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiisamu ya Palestina HAMAS amemshukuru Sheikh Ravil Ainuddin na Waislamu wote wa Russia kwa himaya na uungaji mkono wao  kwa kadhia ya Palestina pamoja na misimamo yao thabiti kuhusiana na Palestina.