Faisal al-Miqdad: Erdoğan anataka kusambaza magaidi kaskazini ya Syria
Waziri wa mambo ya nje wa Syria amesema, lengo la rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki la kuanzisha ukanda wa usalama kaskazini ya Syria ni kuweka magaidi katika eneo hilo.
Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki ambaye amekariri mara kadhaa dai la kutaka kupambana na magaidi katika mpaka wa pamoja wa nchi yake na Syria, mnamo mwishoni mwa mwezi uliopita wa Mei alitangaza kuwa nchi yake imekusudia kukamilisha haraka uanzishaji wa ukanda wa usalama wenye urefu wa kilomita 30 kwenye mpaka wa pamoja na Syria.
Waziri wa mambo ya nje wa Syria Faisal al-Miqdad amekosoa vikali sisitizo hilo la kila mara la Erdoğan la kuanzisha ukanda wa usalama katika eneo la kaskazini ya Syria na kueleza kwamba lengo la rais wa Uturuki katika kuchukua hatua hiyo ni kuwaweka na kuwaimarisha magaidi katika eneo hilo la kaskazini ya Syria.
Al-Miqdad amesema, Erdoğan anafanya juu chini kuhakikisha anawasambaza kaskazini ya Syria magaidi aliokuwa amewapatia mafunzo huko nyuma na akaongezea kwa kusema: "tunazitaka nchi zote zisiunge mkono uchu wa kujivutia upande wake alionao Erdoğan".
Operesheni za kijeshi za kinyume cha sheria zilizoanzishwa na jeshi la Uturuki tangu miaka takriban miwili na nusu iliyopita katika ardhi za Syria na Iraq, zimekuwa zikilaaniwa na serikali, wananchi wa nchi hizo pamoja na jamii ya kimataifa, wakitaka kusitishwa operesheni hizo; na askari wa Uturuki kuondoka katika nchi hizo, lakini Ankara ingali inaendeleza operesheni zake hizo za kijeshi katika ardhi za Syria na Iraq kwa kisingizio cha kupambana na magaidi.../