Qatar yaishtaki Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC)
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i91452-qatar_yaishtaki_israel_katika_mahakama_ya_kimataifa_ya_jinai_(icc)
Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imewasilisha mashtaka kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kuhusu kuuliwa shahidi ripota wake, Shireen Abu Akleh, mauaji yaliyofanywa na wanajeshi wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 08, 2022 06:17 UTC
  • Qatar yaishtaki Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC)

Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imewasilisha mashtaka kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kuhusu kuuliwa shahidi ripota wake, Shireen Abu Akleh, mauaji yaliyofanywa na wanajeshi wa Israel.

Wanajeshi wa Israel tarehe 11 Mei mwaka huu walimuuwa kikatili ripota na mwandishi habari wa Kipalestina Shireen Abu Akleh aliyekuwa akiifanyia kazi mtandao wa habari wa al Jazeera ya Qatar katika Ukingo wa Magharibi. Kwa hiyo,  jinai hii kwa hakika ina wadai wawili wa kisheria dhidi ya utawala wa Kizayuni. Wapalestina na televisheni ya Al Jazeera ya Qatar, na wote wana haki ya kufuatilia uhalifu huo. 

Jumuya ya wanahabari wa Palestina pia ilikuwa imewasilisha mashtaka katika mahakama ya ICC huko Hague kuhusu suala hilo kabla ya hatua hii ya televisheni ya al Jazeera.  Hivi sasa pia timu ya wanasheria wa televisheni ya al Jazeera  ambayo tayari imefanya uchunguzi kamili na wa kina kuhusu faili hilo la mauaji na kupata ushahidi mpya kulingana na simulizi za mashahidi kadhaa, imewasilisha mashtaka yake kwa mahakama ya ICC mjini Hague Uholanzi. Mtandao huo wa habari wa Qatar umeeleza kuwa, video mpya zilizopatikana zinaoyesha waziwazi namna wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel walivyommiminia risasi Shireen Abu Akleh na maripota wenzake. 

Mauaji ya kikatili yaliyofanywa na Israel kwa Shireen Abu Akleh, ripota wa al Jazeera 

Sababu iliyopelekea kuwasilishwa mashtaka haya katika Mahakama ya Kimatafa ya Jinai ni kwamba mauaji ya Shireen Abu Akleh yanahesabiwa kuwa ni jinai ya kivita. Baada ya jinai hiyo, wataalamu wa sheria wa Umoja wa Mataifa walitangaza katika taarifa yao kuwa: "Kuuliwa Shirin Abu Akleh, ripota wa Kipalestina wa Al-Jazeera akiwa amevalia sare ya mwandishi wa habari ni uhalifu wa kivita." 

Si hayo tu, Wapalestina na televisheni ya al Jazeera ya Qatar zinasisitiza kuwa Abu Akleh aliuawa kwa makusudi. Jeshi la srael limekiri kwamba, jinai hiyo ilifanywa na wanajeshi wa Israel lakini linadai kuwa haikuwa ya makusudi. Nukta nyingine ni kuwa katika taarifa yake ya mwezi Februari mwaka 2021, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ilitangaza kuwa inayo mamlaka ya kufuatilia jinai mbalimbali zinazojiri katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina. Ni kwa kuzingatia sababu hizo, ndio maana Wapalestina na Waqatar wakawalisha mashtaka yao katika mahakama hiyo.

Shahidi Shireen Abu Akleh, ripota aliyeuliwa kinyama na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni akiwa kazini 

Hatua hiyo ya al Jazeera imekabiliwa na radiamali ya Israel na Marekani. Kufuatia mashtaka hayo yaliyowasilishwa na al Jazeera, Avgdor Lieberman Waziri wa Fedha wa Israel ametaka kusitishwa matangazo ya mtandao huo wa Qatar katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel). Naye Yair Lapid waziri mkuu anayeondoka madarakani wa Israel ameeleza kuwa, hakuna mtu anayeweza kuwawajibisha wanajeshi wa Israel. Serikali ya Marekani pia imepinga hatua ya kuwasilishwa ICC faili la kesi hiyo. Ned Price Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani amesema kuhusu upinzani wa nchi yake dhidi ya hatua yoyote ya mahakama ya ICC kuchunguza utawala wa Kizayuni kufuatia mauaji ya Shireen Abu Akleh ambaye pia alikuwa na uraia wa Marekani kwamba: Washington inapinga hatua hiyo.

Avigdor Lieberman, Waziri wa Fedha wa utawala haramu wa Israel 

Baada ya kuwasilishwa kesi hiyo ya mauaji ya mwandishi huyo wa habari wa Kipalestina kwenye mahakama hiyo, taasisi hiyo ya kimataifa inapasa kwanza kufanya uchunguzi katika uwanja huo na kisha kuwatambua wahusika wa jinai hiyo na kuwaadhibu moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Randy Dickson, wakili wa al Jazeera amesisitiza katika mkutano wa waandishi wa habari kwenye makao makuu ya ICC huko Hague nchini Uholanzi kwamba mahakama hiyo inapasa kuwatambua na kuwaadhibu wahusika wa moja kwa moja katika  mauaji ya Abu Akleh. Mahakama hiyo pia ina mamlaka ya kutoa hukumu kwa wale wote walioamuru kutekelezwa jinai hiyo." 

Nukta ya mwisho ni kuwa, hata kama utawala wa Kizayuni kwa mara nyingine tena utahepa kuadhibiwa kwa kukingiwa kifua na Marekani, lakini kama mahakama ya ICC itasikiliza kesi hiyo na kisha  kutoa hukumu yake basi uamuzi huo unaweza kuhesabiwa kuwa ni kufeli pakubwa kisiasa na kisheria kwa Tel Aviv.