HAMAS yafanyia majaribio kombora lake jipya Ukanda wa Gaza
(last modified Tue, 27 Jun 2023 07:38:10 GMT )
Jun 27, 2023 07:38 UTC
  • HAMAS yafanyia majaribio kombora lake jipya Ukanda wa Gaza

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imefanyia majaribio kombora lake jipya katika Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Palestina, majaribio hayo ya kombora jipya la HAMAS yalifanyika jana Jumatatu, ili kuonyesha uwezo na nguvu za kijeshi na kujihami za harakati hiyo ya muqawama wa Kiislamu ya Palestina.

Habari zaidi zinasema kuwa, HAMAS imevurumisha marekoti kadhaa kutoka Pwani ya Gaza, kuelekea kwenye maji ya bahari lililoko magharibi mwa ukanda huo.

Taarifa ya HAMAS imesema lengo la majaribio hayo ni kujiandaa kwa ajili ya makabaliano tarajiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel, na vile vile kuongeza nguvu na kuimarisha uwezo wa makombora ya harakati hiyo ya mapambano.

Haya yanajiri wakati huu ambapo operesheni za ulipizaji kisasi  za makundi ya muqawama ikiwemo HAMAS zimeshtadi, baada ya jeshi la utawala wa Kizayuni Israel kuua na kujeruhi makumi ya Wapalestina katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

HAMAS imetungua pia droni ya Wazayuni

Wakati huohuo, HAMAS imesema katika taarifa kuwa, matamshi ya kiuhasama na kiuadui ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina yanaonesha dhati ya ufashisti ya utawala huo wa Kizayuni.

HAMAS imesema, "Mtazamo wa Netanyahu unaweka wazi malengo ya utawala huo wa kifashisti kwa kutumia mauaji ya kimbari, uangamizaji wa kizazi na ukoloni wa walowezi wa Kizayuni."

Netanyahu karibuni aliiambia Kamati ya Masuala ya Nje ya Bunge la Israel (Knesset) kwamba, utawala huo pandikizi unapasa kuangmiza kikamilifu azma na ndoto ya Wapalestina ya kujiundia taifa huru.

Tags