UN: Israel inafanya ukatili dhidi ya watoto wa Palestina
Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake kuhusu ukatili unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watoto wa Kipalestina.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq ameashiria ukatili mkubwa unaofanywa na utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina na kusema: Umoja huo utafanya uchunguzi kuhusu ukatili huo hususan ule unaofanywa dhidi ya watoto wadogo.
Farhan Haq ameongeza kuwa, Umoja wa Mataifa pia utafuatilia mauaji ya Mahmoud Badran, kijana wa Kipalestina aliyekuwa na umri wa miaka 15 ambaye alipigwa risasi na askari Israel wanaodai walimuua shahidi kwa makosa.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa pia amesema kuhusu suala la kupunguzwa kiwango cha maji ya maeneo ya kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi yakiwemo yale ya Nablos na Turkarm kwamba ujumbe wa Palestina umewasilisha maombi katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kwa Katibu Mkuu wa umoja huo na kwamba mwakilishi wa UN huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu atafuatilia jambo hiko ipasavyo.
Shirika la Maji la Israel limekata asilimia 50 ya maji ya kunywa ya Wapalestina wanaoishi katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi, suala ambalo limewazidishia masaibu katika kipindi hiki cha joto kali na kwnye mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.