Papa Francis: Kuivunjia heshima Qurani ni ukatili
Kwa mara nyingine tena Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amelaani vitendo vya karibuni vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Sweden na Denmark na kusisitiza kuwa, vitendo hivyo vya kudhalilisha matukufu ya kidini havina tofauti na ukatili.
Papa Francis amesema hayo katika barua yake ya jana Jumanne, akijibu barua aliyoandikiwa na mwanachuoni wa Kishia wa Argentina, Abdul Karim Paz, ambaye ni Mjumbe wa Wakfu wa Kiislamu katika nchi hiyo ya Amerika ya Latini.
Papa amesema ameghadhabishwa na kukerwa na vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu huko nchini Sweden na Denmark, huku akitilia mkazo suala la wafuasi wa dini mbalimbali kuishi pamoja kwa amani na maelewano, sanjari na kupinga misimamo na mitazamo ya kufurutu mipaka.
Sehemu moja ya barua ya Papa inasema: Tukio la kuchomwa moto Qurani Tukufu ni kitendo cha kikatili. Vitendo hivyo vinaumiza na kuzuia mazungumzo pevu baina ya watu.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani amesema kuwa, uhuru wa maoni na kujieleza haipasi kuonekana kama idhini ya kitendo hicho cha fedheha cha kuvunjia heshima matukufu ya dini nyingine.
Wiki iliyopita, mwanachuoni wa Kishia wa Argentina, Abdul Karim Paz alimuandikia barua Papa, akisisitiza kuwa wanaochoma moto Qurani Tukufu wapo dhidi ya umoja wa dini za Nabii Ibrahim AS.
Waislamu kote duniani wameendelea kupaza sauti zao kulalamikia kitendo hicho kiovu cha kudhalilisha na kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu nchini Sweden na Denmark, huku kampeni kubwa ya dunia nzima ya kususia bidhaa zinazozalishwa na nchi hizo za Magharibi ikishika kasi.