Aug 04, 2023 07:45 UTC
  • Kiongozi wa kundi la kigaidi la MKO apigwa marufuku kuingia Albania

Albania imempiga marufuku kiongozi wa kundi la kigaidi la Munafiqin (MKO) kutia mguu katika ardhi ya nchi hiyo ya Ulaya.

Duru za habari zinaarifu kuwa, mamlaka za Albania zimempiga marufuku Maryam Rajavi, kinara wa MKO kuingia nchini humo, baada ya kupitia nyaraka zilizoashiria kuwa kundi hilo la Munafiqin limehusika na hujuma za kigaidi nchini Iran.

Haya yanajiri wiki chache baada ya polisi ya Albania kuvamia makao makuu ya kambi ya kundi la kigaidi la Munafiqin kufuatia amri ya Mahakama Kuu ya nchi hiyo. Rajavi alitorokea Ufaransa baada ya kujiri tukio hilo.

Katika operesheni hiyo ya Juni 20, polisi ya Albania ilielekea katika kambi ya Ashraf-3 kwa ajili ya kufanya uchunguzi kwa mujibu wa agizo la Mahakama Kuu ya kupambana na ugaidi ya nchi hiyo.

Vyombo vya usalama vya Albania vilitangaza kuwa hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na hatua za uhalifu na ugaidi zinazofanywa na kundi hilo. 

Kundi la kigaidi la Munafiqin limehusika katika mauaji ya zaidi ya Wairani elfu 17 wakiwemo wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, viongozi wa angazi ya juu wa serikali na raia wa kawaida wasio na hatia na pia raia wa nchi za nje. 

Tags