Wasomi UK: Kushambulia Qur'ani ni uchupaji mipaka
Wasomi mashuhuri nchini Uingereza wamelaani vitendo vya kuchoma moto Qur'ani Tukufu katika nchi za Scandinavia na kusisitiza kuwa, vitendo hivyo vya uchupaji mipaka vinapaswa kukomeshwa.
Wanaakademia hao maarufu katika fani za jamii, dini na imani nchini Uingereza wameeleza bayana kuwa, kuendelea vitendo vya kuchomwa moto Kitabu Kitukufu cha Waislamu ni jambo lisilokubalika.
Alison Scott-Baumann, Profesa wa Masomo ya Jamii na Dini katika Taasisi ya Mafunzo ya Kiislamu ya Chuo Kikuu cha SOAS amenukuliwa na shirika la habari la Anadolu akisema kuwa, vitendo vya kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu hasa katika nchi za Denmark na Sweden vimechochewa na kushajiishwa na wanasiasa wa nchi hizo.
Ameeleza bayana kuwa, "Serikali ya kidemorasia inapaswa kutofautisha baina ya uhuru wa kujieleza na uchochezi wa makusudi. Ni wazi vitendo hivi (vya kuvunjia heshima Qur'ani) ni vya kichochezi."
Naye David Thomas, Profesa wa Tiolojia na Dini katika Chuo Kikuu cha Birmingham ameiambia Anadolu kuwa, vitendo vya kuishambulia Qur'ani vinafanywa na watu wenye misimamo mikali ya kufurutu ada.
Amesema wanaofanya vitendo hivyo vilivyo dhidi ya Uislamu na Waislamu, wanafahamu vyema kuwa hatua zao hizo hasa kuchoma moto Qur'ani zitaamsha hasira na kuchochea hisia za mabilioni Waislamu.