Rais Xi wa China 'kutoshiriki' mkutano ujao wa kundi la G20
Wizara ya Mambo ya Nje ya China imesema Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Li Qiang ataongoza ujumbe wa taifa hilo katika mkutano ujao wa kundi la G20 nchini India, hatua inayoashiria kuwa Rais Xi Jinping hatoshiriki kongamano hilo.
Mao Ning, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China alisema hayo jana Jumatatu na kuongeza kuwa: G20 ni jukwaa kuu la ushirikiano wa kiuchumi duniani, na China daima imekuwa ikilichukulia kwa uzito suala la kushiriki mikutano ya aina hii.
Hata hivyo wadadisi wa mambo wanaamini kuwa, hatua ya Xi kutohudhuria mkutano huo ni njia nyingine ya Rais huyo wa China kukwepa taasisi za kimataifa zinazotawaliwa na Marekani.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China hakukanusha au kuthibitisha matamshi ya waandishi wa habari waliouliza iwapo kushiriki Waziri Mkuu Li Qiang kwenye mkutano huo kunamaanisha kuwa Rais Xi hatohudhuria.
Kongamano hilo la Kundi la G20 la nchi 20 zilizostawi kiviwanda duniani linatazamiwa kufanyika New Delhi, mji mkuu wa India baina ya Septemba 9 na 10.
Tangu kufanyika kwa duru ya kwanza ya mkutano wa G20 mwaka 2008, hakuna Rais wa China aliyekosa kushiriki mikutano hiyo, ingawaje Xi alishiriki mikutano ya mwaka 2020 na 2021 kwa njia ya intaneti kutoka na janga la Corona.
Russia pia itawakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo kwenye mkutano huo, kutokana na waranti wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) dhidi ya Rais Vladimir Putin.
Wen-Ti Sung, mtaalamu wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Australia amesema sio sadfa kwa Xi kutoshitiki mkutano wa G20, mwezi mmoja baada ya kushiriki kwenye mkutano wa kundi la BRICS nchini Afrika Kusini.
Amesema: Xi kutoshiriki klabu ya madola makubwa ya Magharibi baada ya kushiriki kongamano la BRICS huenda kunaashiria msimamo wake kwamba; Mashariki inainukia, na Magharibi inaanguka; na pia anataka kuonyesha mshikamano na Rais Putin wa Russia ambaye pia hatashiriki.