Kukita mizizi ubaguzi katika kikosi cha polisi Marekani
(last modified Fri, 29 Sep 2023 12:46:51 GMT )
Sep 29, 2023 12:46 UTC
  • Kukita mizizi ubaguzi  katika kikosi cha polisi Marekani

Kwa mujibu wa wataalamu wa Umoja wa Mataifa, ubaguzi wa rangi uliokithiri unaonekana katika vikosi vya polisi na mfumo wa mahakama wa nchini Marekani.

Tafiti zinaonyesha kuwa tatizo la ubaguzi wa rangi katika kikosi cha polisi Marekani ni zaidi ya madai  kuwa idadi ya maafisa wa polisi wenye misimamo ya kibaguzi nchini humo ni ndogo.

Idadi ya raia waliouliwa na polisi wa Marekani  katika kipindi cha  hivi karibuni  ni zaidi ya jumla ya mauaji ambayo polisi katika nchi nyingine hufanya katika kipindi cha mwaka mmoja.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB; Wataalamu wa Umoja wa Mataifa walitangaza katika ripoti kwamba: "Ubaguzi wa rangi nchini Marekani, urithi wa utumwa, biashara ya utumwa na miaka mia moja ya utawala wa kibaguzi uliohalalishwa baada ya kukomeshwa kwa utumwa unaendelea kuwepo leo hii."

Kwa mujibu wa ripoti hiyo,  watu weusi au wenye asili ya Afrika wanakabiliwa na hatari ya kuuliwa na polisi wa Marekani mara tatu zaidi kuliko watu weupe.

Wataalamu wa masuala ya kijamii nchini Marekani wametoa wito kwa watu wote  zikiwemo idara za polisi na vyama vya wafanyakazi kupambana na suala la kutojali sheria.

Ripoti hiyo, imetoa mapendekezo 30 kwa serikali ya Marekani na idara za polisi nchini humo.

Wataalam hao wamesema wamehisi ukosefu mkubwa wa imani kwa serikali miongoni mwa watu wenye asili ya Kiafrika katika kutekeleza sheria na mifumo ya haki ya masuala ya jinai, hasa kutokana na unyanyasaji wa kihistoria na unaoendelea wa polisi na hisia za ukandamizaji wa kimfumo na kutokujali kuhusu ukiukwaji huu.

Ripoti hiyo inataja kesi za kutia wasiwasi sana za watoto wenye asili ya Kiafrika waliohukumiwa kifungo cha maisha jela, wajawazito waliofungwa minyororo wakati wa kujifungua na watu waliowekwa katika vifungo vya upweke kwa miaka kumi. 

Pia umeelezea jinsi baadhi ya watu wanavyokabiliwa na kazi za kulazimishwa katika magereza jasa za mashambani, ambao ni aina ya utumwa wa kisasa.

Inasemekana kuwa ubaguzi wa rangi nchini Marekani, nchi inayodai kuheshimu haki za binadamu, umekithiri  kwa kiasi kwamba athari za siasa hizo zinaonekana wazi  katika taasisi mbalimbali za utendaji na  kisheria nchini humo.

Kila mwaka makumi ya raia Wamarekeni wenye asili ya Afrika huuliwa kidhulma na polisi katika majimbo mbalimbali ya nchi hiyo. Idadi ya wazungu wanaouliwa na polisi ikilinganishwa na wenye asili ya Afrika ni 13 kwa mmoja.

Mamia ya makala yameandikwa  kukosoa hali hii na suala la ubaguzi wa rangi katika jeshi la polisi   kujadiliwa kwa maelfu ya masaa  kwenye televisheni, redio na vyombo vya kisheria .