Amnesty International yataka kuondolewa mzingiro Ghaza
Shirika la Msamaha Duniani (Amnesty International) limetaka kuondolewa mzingiro dhidi ya Ukanda wa Ghaza.
Amnesty International imetangaza kuwa utawala wa Kizayuni unapasa kuhitimisha mzingiro dhidi ya Ukanda wa Ghaza ili huduma za maji na umeme na misaada ya kibinadamu iweze kupatikana kwa ajili ya raia wa eneo hilo.
Kabla ya takwa hili la Amnesty International, Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni, alipiga marufuku kuingizwa vyakula vya aina yoyote, dawa za matibabu, fueli, umeme na hata maji katika Ukanda wa Ghaza sambamba na kuwepo amri ya kutekelezwa mzingiro wa pande zote dhidi ya eneo hilo.
Wanamapambano wa Palestina katika kujibu jinai za kila uchao za Wazayuni; wameanzisha oparesheni ya pande zote kwa jina la "Kimbunga cha al Aqsa" tangu tarehe 7 mwezi huu kuanzia Ukanda wa Ghaza dhidi ya ngome na maeneo ya utawala haramu wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.
Kushindwa vibaya Wazayuni mbele ya wanamapambano wa Palestina, kuangamizwa Wazayuni zaidi ya elfu moja na kupoteza baadhi ya vitongoji na kambi za kijeshi za utawala huo ghasibu kumewapelekea wakuu wa utawala huo katika siku za karibuni kutenda jinai kwa kuanzisha mashambulizi dhidi ya raia na wakazi wa Kipalestina wasio na hatia wa Ukanda wa Ghaza.
Hadi kufikia jana usiku idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi walikuwa karibu elfu tatu huku majeruhi wakiwa elfu 12 na 500; hii ikiwa ni natija ya mashambulizi ya anga ya utawala wa Kizayuni yaliyoanza tangu Oktoba 7 dhidi ya maeneo ya raia, hospitali, vituo vya matibabu na misikiti huko Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.