Jan 02, 2024 10:15 UTC
  • Putin: Ukraine ni kikaragosi tu, Magharibi ndiye adui halisi wa Russia

Rais Vladimir Putin wa Russia amesema, Ukraine yenyewe si adui, lakini vinara wa Magharibi wanaoiunga mkono nchi hiyo ndio maadui halisi wa Russia.

Putin ambaye alikuwa akizungumza katika hospitali ya kijeshi mjini Moscow alikokutana na wanajeshi waliojeruhiwa katika vita vinavyoendelea kati ya Russia na Ukraine ametamka bayana kuwa Ukraine ni kikaragosi tu kilichoko mikononi mwa mataifa ya Magharibi ambacho yanakitumia kupigana na Russia.

Rais wa Russia ameongeza kuwa, vinara wa Magharibi yote ndio maadui halisi wa Russia kuliko Ukraine yenyewe.

Putin amefafanua kwa kusema: “suala si kwamba wanamsaidia adui yetu, bali wao ndio adui yetu. Wanatatua matatizo yao kwa kutumia mikono ya Ukraine, hivyo ndivyo ilivyo hasa".

Ameendelea kueleza kuwa, mzozo kati ya Moscow na Kiev ulipangwa na vinara wa Magharibi, ambao wanapigania kuishinda Russia. Hata hivyo, Magharibi yote kwa pamoja haijaweza kufikia malengo yake, na kushindwa huko tayari kunaonekana kwa kubadilika matamshi inayotoa kuhusiana na mzozo huo.

Rais wa Russia akizungumzia na wanajeshi waliojeruhiwa vitani

Rais wa Russia amekumbusha kuwa wale ambao hadi jana tu walikuwa wakizungumzia haja ya kuiumiza Russia kwa ‘ushindi wa kimkakati’ sasa wanatafuta maneno ya kusema ili kumaliza mzozo huo haraka.

Amesisitiza kwa kusema: "sisi tunataka kumaliza mzozo, tena haraka iwezekanavyo, lakini ni kwa masharti yetu tu. Hatuna hamu ya kupigana milele, lakini pia hatutaachana na msimamo wetu".

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Russia, zaidi ya wanajeshi 380,000 wa Ukraine wameuawa au kujeruhiwa katika vita vinavyoendelea. Aidha, Ukraine imepata hasara kubwa ya vifaa, ambapo takribani mizinga 14,000 na magari mengine ya kivita ya nchi hiyo yameteketezwa. Takwimu hizo za Russia zinaonyesha kuwa, kati ya wanajeshi wote hao waliouawa na kujeruhiwa, 160,000 miongoni mwao wameuawa wakati wa operesheni za Kiev za kujibu mashambulio na kukomboa maeneo yake yanayoshikiliwa na Moscow, ambazo zilianzishwa mapema Juni mwaka jana.../

Tags