Islamabad yaituhumu Kabul sambamba na kufanyika juhudi za kupunguza mivutano
Sambamba na kufanyika safari ya Mkuu wa chama cha Jamiat Ulamae Pakistan na mazungumzo yake na maafisa wakuu wa kundi la Taliban la Afghanistan kwa lengo la kupunguza mivutano, Waziri Mkuu wa Serikali ya Mpito ya Pakistan kwa mara nyingine tena amedai kuwa ardhi ya Afghanistan inatumiwa na maadui dhidi ya Pakistan.
Anwar Haq Kakar, Waziri Mkuu wa Serikali ya Mpito ya Pakistan, amesema kuwa ardhi ya Afghanistan haipaswi kuwa tishio kwa Pakistan na nchi nyingine za eneo hilo, na kuongeza kuwa serikali yenye makao makuu yake mjini Kabul inapaswa kulipa kipaumbele suala hilo.
Tokea kuachukua tena madaraka Taliban nchini Afghanistan mwezi Agosti 2021, maeneo ya mpaka wa Afghanistan na nchi jirani, hasa Pakistan, yameshuhudia makumi ya mashambulizi ya kigaidi. Katika shambulizi la kigaidi la Jumatatu iliyopita dhidi ya vikosi vya usalama vya Pakistan katika mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa kaskazini mwa nchi hiyo, watu 5 waliuawa na wengine 10 kujeruhiwa. Pakistan inadai kuwa uungaji mkono wa kundi la Taliban la Afghanistan kwa kundi la Pakistan la Tehreek-e-Taliban kwa upande wa pili wa mpaka ni chanzo cha kushadidi mashambulizi hayo, lakini Taliban inapinga madai hayo na kusema Pakistan imechukua uamuzi wa kuwafukuza wahamiaji wa Afghanistan na kuishinikiza serikali ya Taliban kwa kisingizio cha uungaji mkono wa Kabul kwa kundi la Tehreek-e-Taliban la Pakistan.
Katika maelezo yake kuhusiana na jambo hilo, Waziri Mkuu wa Pakistan amesisitiza kuwa uamuzi huo ni wa wananchi walio wengi wa Pakistan na kuwa wakimbizi wasiokuwa na hati za utambulisho hawapaswi kukaa katika nchi nyingine kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Matamshi ya Waziri Mkuu wa Pakistan kuhusu tishio la Afghanistan katika ardhi ya nchi hiyo na suala la kufukuzwa wakimbizi wa Afghanistan yametolewa wakati ambapo Fazal Rehman, Mkuu Chama cha Jamiat Ulemaa cha Pakistan, alisafiri mjini Kabul mapema wiki hii na kukutana na viongozi wa Taliban kwa ajili ya kupunguza mivutano iliyopo kati ya Kabul na Islamabad. Kwa kuzingatia uamuzi wa kiongozi wa Taliban wa kukataa kukutana na Fazlur Rahman na sisitizo jingine la Waziri Mkuu wa Pakistan kuwa Afghanistan ni tishio kwa ardhi ya nchi hiyo, inaonekana kuwa safari ya kongozi huyo wa Pakistan mjini Kabul haikuwa na natija chanya katika kupunguza mzozo uliopo kati ya pande hizo mbili.
Idara ya Usalama ya Pakistan ilitangaza wiki iliyopita kuwa zaidi ya operesheni 18,000 za kijasusi zilitekelezwa na nchi hiyo mwaka jana, na kusisitiza kwamba vitisho vingi vya usalama vilitokea Afghanistan na kwamba operesheni hizo zilipelekea kuawa magaidi wasiopungua 566 na mamia ya askari usalama na raia wa nchi hiyo.
Hii ni katika hali ambayo maafisa wakuu wa Taliban mara kadhaa wamekuwa wakikanusha shutuma za Islamabad na kusisitiza kwamba suala la Tehreek-e-Taliban Pakistan (TTP) ni tatizo la ndani la Islamabad, na kuwa Pakistan inapaswa kulitatua yenyewe.
Bila shaka suala la kuwepo makundi ya kigaidi nchini Afghanistan si madai ya Pakistani pekee, bali nchi nyingine kama vile India, Iran, Tajikistan na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mara kadhaa zimekuwa zikieleza wasiwasi wao kuhusu kuwepo makundi ya kigaidi katika nchi hiyo. Ingawa Taliban inadai kwamba hakuna tishio kwa nchi jirani kutoka eneo la Afghanistan, lakini kwa mtazamo wa Pakistan na majirani wengine wa Afghanistan, serikali ya nchi hiyo, ina jukumu la kimataifa la kushughulikia usalama wa nchi jirani pamoja na kuthibitisha kivitendo madai yake ya kuimarisha amani wa utulivu nchini humo. Suala hilo ndio sababu kuu ya kutokea hitilafu za mitazamo kati ya Taliban na Pakistan.