Feb 20, 2024 12:53 UTC
  • Russia: Makubaliano ya JCPOA hayana mbadala wake

Balozi na Mwakilishi wa Russia katika taasisi za kimataifa zenye makao huko Vienna nchini Austria amesema njia pekee ya kuyahuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni kuyarejesha katika hali yake ya asili.

Mikhail Ulyanov amesema hayo leo Jumanne katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X (Twitter) na kusisitiza kuwa, JCPOA haina chaguo mbadala na kwamba dhana ya kutaka kuandikwa upya mapatano hayo ni njozi.

Ulyanov amebainisha kuwa, Russia inataka kuona makubaliano hayo ya kimataifa yanarejea katika hali yake ya mwanzo, pasi na kupunguzwa au kuongezewa kitu chochote.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Russia ameitaka Marekani iiondolee vikwazo sekta ya mafuta ya Iran ili makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ambayo Washington ilijiondoa kwayo Mei mwaka 2019 yaendelee kutekelezwa.

Mwakilishi wa Russia katika taasisi za kimataifa zenye makao huko Vienna nchini Austria amesisitiza kuwa, hakuna mbadala wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Mikhail Ulyanov, mwadiplomasia wa ngazi ya juu wa Russia

Serikali Rais Joe Biden wa Marekani licha ya kukiri kufeli sera za mashinikizo ya kiwango cha juu za serikali ya kabla yake dhidi ya Iran, lakini mpaka sasa haijachukua hatua ya maana ya kuirejesha Washington katika mapatano hayo ya kimataifa.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa upande wake inasisitiza kuwa, itafungamana tena kikamilifu na majukumu yake kwa mujibu wa mapatano hayo ya nyuklia pale Marekani nayo itakapoiondolea nchi hii vikwazo vya upande mmoja. 

Tags