May 04, 2024 09:53 UTC
  • WHO yataka mataifa yakamilishe mkataba wa kudhibiti majanga

Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ameyataka mataifa ya dunia yakamilishe mkataba wa kudhibiti majanga.

Tedros Adhanom Ghebreyesus Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ameyataka mataifa ya dunia kuridhia makubaliano ya kusaidia kupambana na miripuko ya magonjwa katika siku za usoni, ikiwa ni baada ya athari kubwa za janga la Covid-19.

Akizungumza mjini Geneva Uswisi kkiongozi huyo wa WHO amehimiza nchi ambazo hazikukubali kikamilifu kwa maandishi zijiepushe kuzuia maafikiano kati ya mataifa 194 wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ili ulimwengu upate nusura.

Manesi wakitoa huduma kwa mmoja wa wagonjwa katika kipindi cha mripuko wa maradhi ya Covid-19

 

Taarifa zaidi zinasema kuwa, mkataba mpya na mfululizo wa marekebisho ya kisheria katika kushughulika na miripuko unakusudiwa kusaidia ulinzi wa ulimwengu dhidi ya vimelea vipya vya magonjwa ya mripuko baada ya janga la COVID-19 kuua mamilioni ya watu.

Inaelezwa kuwa, nchi za dunia zinatakiwa kukamilisha haraka mchakato wa mazungumzo kuhusiana na makubaliano hayo ifikapo tarehe 10 ya mwezi huu wa Mei, kwa minajili ya kuipitisha katika mkutano wa kila mwaka wa Shirika la Afya Duniani (WHO) baadae mwezi huu, lakini vyanzo vinavyohusika vinasema kuwa, bado kuna tofauti kubwa zilizosalia ambazo zinapaswa kumalizwa na kuandaa mazingira ya kufikiwa makubaliano hayo.