May 09, 2024 07:09 UTC
  • AstraZeneca imeondoa sokoni chanjo yake ya Covid-19

Kampuni kubwa ya Madawa ya AstraZeneca imeliomba rasmi Shirika la Madawa la Ulaya kuondoa idhini yake ya chanjo ya COVID-19.

Katika sasisho kwenye wavuti wa Wakala wa Dawa wa Ulaya jana Jumatano, mdhibiti wa wakala huo ameeleza kuwa idhini ya chanjo ya Uviko-19 ya Vaxzevria ya Kampuni ya AstraZeneca imeondolewa kwa ombi la mmiliki wa idhini ya uuzaji.

Chanjo hiyo ya Uviko-19 ambayo awali iliidhinishwa mwezi Januari 2021 ilikabiliwa na wasiwasi wa usalama kuhusu kuganda kwa damu kwa nadra, na hivyo kuzipelekea nchi mbalimbali kusitisha matumizi yake kwa muda.

Hali ya wasiwasi na kuitilia shaka chanjo hiyo ya Covid-19 ya kampuni ya Astrazeneca ilidumu licha ya Mdhibiti wa Umoja wa Ulaya kusema kuwa hatari jumla inayoweza kusababishwa na chanjo hiyo ni ya kiwango kidogo. 

Itakumbukwa kuwa dunia ilipoathiriwa na janga la Corona, mabilioni ya dozi za chanjo ya Astrazeneca yalisambazwa katika nchi maskini kupitia programu iliyoratibiwa na Umoja wa Mataifa kwa sababu ilikuwa nafuu na rahisi zaidi kuzalisha na kusambaza.

Uviko-19 

Hata hivyo tafiti baadaye zilipendekeza kuwa chanjo za RNA zilizotengenezwa na Pfizer-BioNTech na Moderna zinatoa ulinzi bora dhidi ya Covid-19 na anuwai zake nyingi.

 

Tags