Jan 16, 2024 06:54 UTC
  • China yatoa tahadhari ya kuibuka tena mripuko wa COVID-19 kupitia spishi ya aina nyingine

Maafisa wa Afya nchini China wametahadharisha juu ya uwezekano wa kuibuka tena mripuko wa ugonjwa wa COVID-19 katika mwezi huu wa Januari, utakaochochewa na kuongezeka maambukizi ya spishi mpya ya JN.1.

Ingawa kesi za maambukizi zilizopo hivi sasa ni za kiwango cha chini, na kiwango cha vipimo vilivyofanywa katika vituo vya uchunguzi ni chini ya asilimia moja, Tume ya Taifa ya Afya ya China (NHC) imetoa indhari ya ongezeko la uwepo wa spishi hiyo ya JN.1.

Wang Dayan, Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Mafua cha China, ameeleza katika mkutano wa waandishi wa habari wa NHC ya kwamba, wataalamu wamefikia hitimisho kuwa aina mbalimbali za magonjwa ya kupumua zitaenea wakati wa majira ya baridi na msimu wa mapukutiko wa mwaka huu, na kati yao, virusi vya mafua itakuwa sababu kuu ya maradhi hayo.

Wang amehusisha ongezeko la spishi ya JN.1 na sababu kadhaa ikiwa ni pamoja watu wenye maambukizi walioingia China kutokea nje ya nchi, viwango vya chini vya maambukizi ya mafua na kupungua kinga ya mwili.

Mamlaka ya udhibiti wa magonjwa ya Marekani imekadiria kuwa spishi ya JN.1 tayari inachangia karibu asilimia 62 ya kesi nchini kote, na pia inaongoza barani Ulaya.

Licha ya kuwepo kiwango cha chini cha maambukizi ya COVID-19, hospitali za China zinajiandaa kwa uwezekano wa kutokea mripuko. Wang Guiqiang, mkuu wa idara ya magonjwa ya kuambukiza katika Hospitali ya Kwanza ya Chuo Kikuu cha Peking, amesema, wanajiandaa kuchukua hatua kadhaa ikiwemo utoaji wa programu za mafunzo, kuongeza usambazaji wa rasilimali watu na kutumia teknolojia ili kurahisisha michakato.

Aidha, Wang ameshauri makundi yaliyo katika hatari kubwa zaidi ya maambukizi kama vile wanawake wajawazito, watoto na wazee wanapaswa kuipa kipaumbele chanjo ya mafua ya kila mwaka na kudumu kuwa katika mazingira mazuri ya kiafya.../

 

 

Tags