May 10, 2024 02:09 UTC
  • Yemen yashambulia meli 3 za Waisraeli katika Ghuba ya Aden, Bahari ya Hindi

Msemaji wa Jeshi la Yemen amesema vikosi vya jeshi la majini, anga na makombora vya nchi hiyo vimezishambulia meli tatu zenye uhusiano na Israel kama sehemu ya kampeni ya baharini ya kuwaunga mkono na kuwatetea Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Akizungumza jana Alhamisi kupitilia televisheni ya taifa, msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree alitangaza kuwa vikosi vya jeshi la nchi hiyo vimelenga meli mbili za MSC DIEGO na MSC GINA, katika maji ya Ghuba ya Aden kwa makombora kadhaa ya balestiki na ndege zisizo na rubani.

Brigedia Jenerali Saree amesema, meli ya MSC VITTORIA pia ilishambuliwa mara mbili, katika Bahari ya Hindi na katika Bahari ya Arabia.

Msemaji wa Jeshi la Yemen ameongeza kuwa: "Jeshi letu linafuatilia matukio ya Ukanda wa Gaza na halitasita kuzidisha operesheni zake za kukabiliana na ukandamizaji unaofanywa dhidi ya watu wa Palestina."

Amesisitiza kuwa, Jeshi la Yemen litaendelea kuzuia harakati za baharini za Israel hadi utawala huo ghasibu utakapokomesha hujuma zake dhidi ya watu wa Gaza na kuondoa mzingiro wake katika ardhi ya Palestina.

Israel ilianzisha vita na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza Oktoba 7 mwaka jana ikiungwa mkono na kusaidiwa na nchi za Magharibi hususan Marekani. 

Utawala wa Tel Aviv hadi sasa umewauwa Wapalestina karibu elfu 35, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na wengine 78,404 wamejeruhiwa.

Tags