Serikali: Uchaguzi wa rais wa Iran utafanyika ndani ya siku 50
Msemaji wa Baraza la Kulinda Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema baraza maalumu litaundwa kwa ajili ya kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi wa rais katika kipindi cha siku 50 zijazo.
Hadi Tahan Nazif, Msemaji wa Baraza la Kulinda Katiba ya Iran amesema baraza hilo litajumuisha Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge), Mkuu wa Idara ya Mahakama na maafisa wengine wa ngazi za juu wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu.
Amesema kwa mujibu wa Katiba ya Iran, Mohammad Mokhber, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiye atakayekaimu nafasi ya Rais Sayyid Ebrahim Raisi aliyeaga dunia katika ajali ya helikopya jana Jumapili.
Nazif amesema Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ataiongoza serikali akishapasishwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei.
Msemaji wa Baraza la Kulinda Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hakutakuwa na ombwe la uongozi hapa nchini, na kwamba kipindi cha mpito na mchakato wa kukabidhiana madaraka utafanyika kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.
Baraza la Mawaziri limeeleza kuwa litalijuilisha taifa adhimu na aminifu la Iran kuhusu wakati na mahali itakapofanyika shughuli ya kuaga mwili wa Rais Raisi aliyekufa shahidi pamoja na miili ya mashahidi wengine walioandamana naye.