Iran yaendelea na jitihada za kusimamishwa vita Ghaza na Lebanon
(last modified Thu, 31 Oct 2024 07:11:42 GMT )
Oct 31, 2024 07:11 UTC
  • Iran yaendelea na jitihada za kusimamishwa vita Ghaza na Lebanon

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefanya mazungumzo na mawaziri wenzake wa mambo ya nje wa Misri, Indonesia na Qatar na kujadiliana nao masuala ya kikanda na uhusiano wa pande mbili ikiwa ni muondelezo wa jitihada za Iran za kuhakikisha vita vinakomeshwa huko Ghaza na Lebanon.

Mtandao wa Sahab umelinukuu Shirika la Habari la Wanachuo wa Iran (ISNA) likitangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi amefanya mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdul Ati na kusisitiza kuwa, hali ya eneo hili ni ya hatari na ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na zinazofaa zakuhakikisha kunafikiwa usitishaji vita nchini Lebanon na Ukanda wa Ghaza haraka iwezekanavyo.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Misri, pia wameelezea kuridhishwa kwao na mchakato chanya wa mazungumzo kati ya nchi hizo mbili katika miezi ya hivi karibuni, kikiwemo kikao cha marais wa Jamhuri ya Kiislamu ya  Iran na Misri huko Kazan nchini Russia na kusisitizia haja ya kuendelezwa mazungumzo hayo yanayozingatia maslahi ya mataifa hayo mawili.

Aidha Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na waziri mwenzake wa Qatar Sheikh Mohammad bin Abdulrahman Aal Thani kuhusu matukio ya eneo hili na juhudi za kusimamisha mara moja vita huko Ghaza na Lebanon.

Sayyid Abbas Araghchi amefanya mazungumzo ya simu pia na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Indonesia, Sugi Yono na sambamba na kumpongeza kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo, amepongeza pia msimamo madhubuti wa Indonesia katika kulaani vikali uchokozi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran. Pande mbili zimetaka kufanyika juhudi za pamoja za nchi za Kiislamu ili kukomesha jinai za Israel huko Ghaza na Lebanon.

Tags