Viongozi wa dunia wasikitishwa na kifo cha Rais wa Iran
Viongozi wa mataifa mbali mbali duniani wameendelea kutoa mkono wa pole kufuatia vifo vya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Ebrahim Raisi pamoja na wenzake kadhaa katika ajali ya helikopta iliyotokea jana katika mkoa wa Azarbaijan Mashariki, kaskazini magharibi mwa Iran.
Amir wa Qatar, Tamim bin Hamad Al Thani amesema katika taarifa kuwa: Natoa mkono wa pole kwa serikali na taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kufuatia tukio chungu la ajali ya helikopta iliyopelekea kuaga dunia Rais Ebrahim Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje, Hossein Amir-Abdollahian na maafisa wengine waliokuwa wameandamana nao.
Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi amesema amesikitishwa mno na kifo cha Dakta Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesema: Mchango wake katika kuimarisha uhusiano wa India na Iran daima utakumbukwa. Tunasimama na taifa la Iran wakati huu wa majonzi.
Aidha Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammad Shia Al-Sudani ameeleza kusikitishwa kwake na vifo vya Rais wa Iran pamoja na maafisa wengine wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu.
Helikopta hiyo ilikuwa imembeba Raisi Ebrahim Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian, Gavana wa mkoa wa Azarbaijan Mashariki Malek Rahmati, Imam wa Swala ya Ijumaa na mwakilishi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu huko Tabriz, Mohammad Ali Al- Hashem na maafisa wengine kadhaa wa serikali.
Katika risala yake ya rambirambi, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imesema inasimama pamoja na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei, serikali ya Iran, na taifa la Iran kwa ujumla kufutia vifo hivyo vya kusikitisha.
Taarifa hiyo imeipongeza Jamhuri ya Kiislamu kwa kuwapa himaya na kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina, na kusisitiza kuwa Palestina leo hii ni suala la kwanza na la pamoja kwa nchi zote za Kiislamu.
Naye Mohammed Ali Al-Houthi, Mkuu wa Baraza Kuu la Mapinduzi la Yemen amesema katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa X kuwa: Rambirambi zetu kwa taifa na uongozi wa Iran wakati huu wa majonzi. Taifa la Iran litaendelea kufungamana na miongozo ya viongozi wao waaminifu in Sha Allah.
Wakati huo huo, Charles Michel, Rais wa Umoja wa Ulaya amesema EU inatoa mkono wa pole kwa wananchi na serikali ya Iran kufuatia vifo hivyo vya viongozi wa Iran.