May 19, 2024 11:15 UTC
  • Iran yathibitisha imekuwa na mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani

Ofisi ya uwakilishi ya Iran katika Umoja wa Mataifa imethibitisha kuwa kumekuwepo na mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Jamhuri ya Kiislamu na Marekani.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeingia katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani ikiwa imeweza kuzatiti nguvu na uwezo wake wa kieneo katika vita vya Ghaza na kwa kutekeleza operesheni ya mashambulizi ya Ahadi ya Kweli katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Hatua hizo zimechukuliwa sambamba na tahadhari iliyotolewa na Kamal Kharrazi, Mkuu wa Baraza la Mkakati wa Uhusiano wa Nje la Iran, kwamba Tehran itabadilisha sera zake kuu za nyuklia endapo Iran itakabiliwa na vitisho vya aina yoyote ile.
Kharrazi aidha aliitolea mwito Marekani wa kurudi kwenye meza ya mazungumzo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, ofisi ya uwakilishi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa imetoa jibu kwa swali la vyombo vya habari kuhusu habari zilizotangazwa za kufanyika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani nchini Oman, na kutangaza kwamba mazungumzo hayo yamefanyika na yangali yanaendelea.
Kamal Kharrazi

Aidha, Ofisi ya Uwakilishi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa imekumbusha kuwa "mazungumzo hayo si ya mwanzo na wala hayatakuwa ya mwisho".

Awali kabla ya hapo, tovuti ya habari ya Axios ilizinukuu duru mbili za kuaminika za serikali ya Marekani na kutangaza kuwa, wiki iliyopita maafisa wawili waandamizi wa serikali ya Rais Joe Biden, ambao ni Brett McGurk, mshauri mkuu wa Biden katika Asia Magharibi na Abram Paley, kaimu mwakilishi wa Marekani wa masuala ya Iran walifanya mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana na maafisa wa Iran nchini Oman kuhusu jinsi ya kuzuia kupanuka mashambulizi ya kikanda.
Duru ya kwanza ya mazungumzo kama hayo kati ya Marekani na Iran ilifanyika Januari 2024 hukohuko nchini Oman.
Mazungumzo haya ya sasa yamefanyika ukiwa umepita mwezi mmoja tu tangu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipofanya shambulio ambalo halijawahi kutokea la ndege zisizo na rubani na makombora mnamo Aprili 13 dhidi ya vituo vya utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.../

 

Tags